Michezo

Peres Jepchirchir sasa alenga rekodi nyingine katika mbio za marathon

September 8th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

SIKU mbili pekee baada ya kuvunja rekodi ya dunia katika mbio za nusu-marathon, Peres Jepchirchir amejiwekea malengo mapya.

“Sasa naazimia kukimbia marathon chini ya muda wa saa 2:17. Nimeshiriki mashindano mengi ya kilomita 21 na nahisi wakati umefika wa kufanya kitu spesheli katika kivumbi cha marathon. Hata hivyo, haimaanishi kwamba sitawahi kabisa kunogesha tena mbio za kilomita 21,” akaandika Jepchirchir kwenye mtandao wake wa kijamii.

Ili kuweka hai ndoto yake ya kukamilisha marathon kwa muda wa saa 2:17, itamlazimu Jepchirchir kupunguza zaidi ya dakika sita kwenye muda bora wa binafsi wa saa 2:23:53 anaojivunia kwa sasa katika mbio za kilomita 42. Rekodi ya dunia ya saa 2:14:04 katika mbio za marathon kwa wanawake inashikiliwa na Mkenya Brigid Kosgei aliyetawala Chicago Marathon mnamo Oktoba 2019. Alipunguza sekunde 81 kwenye rekodi iliyowekwa na Mwingereza Paula Radcliffe mnamo 2003.

Jepchirchir alivunja rekodi ya kilomita 21 kwa kusajili muda wa saa 1:05:34 katika mbio za RunCzech Half Marathon jijini Prague, Jamhuri ya Czech wikendi iliyopita. Aliiweka rekodi hiyo mpya ya dunia katika uwanja wa Letna Park ambapo alipiga jumla ya mizunguko 16 na nusu na kukimbia umbali wa kilomita 21.097.

Ufanisi huo ulimwezesha kuvunja rekodi ya saa 1:06:11 iliyowekwa na Mwethiopia Netsanet Gudeta mnamo 2018 katika mbio za dunia za kilomita 21 jijini Valencia, Uhispania.

Aliwaongoza Wakenya Brenda Jepleting (1:07:07), Dorcas Jepchumba Kimeli (1:07:14), Edith Chelimo (1:07:16), Sheila Chepkirui (1:07:37) na Vivian Chepkirui (1:09:09) kukamata nafasi sita za kwanza katika mbio hizo zilizodhaminiwa na shirika la RunCzech kwa pamoja na kampuni ya vifaa vya michezo ya Adidas.

Akivalia tena viatu aina ya Adidas Adizero Adios Pro, Jepchirchir aliibuka mshindi wa nishani ya dhahabu katika Nusu-Marathon ya Dunia jijini Cardiff, Uingereza mnamo 2016.

“Hiki ni kiatu kizuri cha kutimka nacho kwenye lami. Ni chepesi sana na kinamwepushia mwanariadha majeraha,” akasema Jepchirchir kwa kusisitiza kwamba atafaulu katika maazimio yake hivi karibuni iwapo atapata waweka kasi wazuri.

“Naamini ningesajili muda wa hata saa 1:04:00 nchini Czech iwapo ningewekewa kasi ya kutosha hadi hatua ya mwisho,” akaongeza Jepchirchir aliyevunja rekodi ya dunia ya saa 1:06:69 iliyowekwa na Mkenya Florence Kiplagat katika mbio za RAK Half Marathon mnamo 2017.

Jepchirchir huishi na mumewe mjini Kapsabet, Kaunti ya Nandi anakofanyia mazoezi. Mama yake mzazi aliaga dunia Jepchirchir akiwa na umri wa miaka miwili pekee. Ni kakaye ndiye alimhimiza zaidi kujitosa katika ulingo wa riadha.