Miili ya wawili yaopolewa kisimani shughuli ya kutafuta wa tatu ikiendelea Ngoingwa
Na LAWRENCE ONGARO
MIILI miwili imetolewa kisimani katika kijiji cha Ngoingwa na idara ya zimamoto ya mji wa Thika huku shughuli ya kutafuta mtu wa tatu aliyezama ikiendelea.
Inadaiwa watu hao watatu waliteleza na kuzama katika kisima hicho mnamo Jumatatu walipokwenda kuchota maji.
Wakazi wa kijiji hicho walisikia makelele ndani ya kisima hicho na kwa haraka wakawaita maafisa wa idara ya zimamoto kutoka mji wa Thika ambao walifika kwa haraka kuwaokoa.
Katika shughuli iliyochukua muda wa saa mbili, wataalamu hao walifanikiwa kutoa miili miwili lakini mmoja ungali kupatikana.
“Tumejaribu tuwezavyo na kuopoa miili miwili ambapo mwili wa tatu bado haujaonekana. Hata hivyo wakazi wa kijiji hiki wanasema kisima hicho kina urefu wa mita 20 kando ya shimo hilo na pengine mtu wa tatu amejikita mle ndani. Hata hivyo, tunafanya kila tuwezalo,” alisema Bw John Warutumo ambaye ni mmoja kati ya waokoaji wa zimamoto Thika.
Naibu kamanda wa polisi katika eneo la Thika Magharibi, Bw Daniel Kitavi, alithibitisha mkasa huo akisema kikosi cha usalama kitafanya juhudi kuona ya kwamba mwili huo uliosalia unapatikana haraka iwezekanavyo.
“Tunatoa wito kwa wakazi wa eneo hili wawe makini wanapochota maji kutoka katika visima,” alisema Bw Kitavi.
Pia walishauriwa wakae mbali na pahala hapo kwani kwa wakati huu ni sehemu hatari.
Wakazi hao wanasema sasa watapata shida ya maji kwa sababu watu wengi walio na maji ya visima huwa wanafunga kwa kufuli.
Miili hiyo miwili imepelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya Thika Level 5 ili kufanyiwa uchunguzi zaidi.