Ruto amuombe Rais msamaha – wabunge
Na CHARLES WASONGA
WABUNGE wanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Usalama wamemtaka Naibu Rais William Ruto kumwomba msamaha Rais Uhuru Kenyatta na familia yake kufuatia hatua ya baadhi ya viongozi wanaosawiriwa kuegemea upande wake kumtusi Kiongozi wa Taifa.
Wakiongozwa na mwenyekiti wa kamati hiyo Paul Koinange, wabunge hao Jumanne wamesema japo Dkt Ruto alilaani hatua ya wabunge Oscar Sudi (Kapseret) na Johanna Ng’eno (Emurua Dikirr) kumkosea Rais heshima, haitoshi kwake kufanya hivyo kupitia mtandao wa Twitter.
“Ni vizuri kwamba Naibu Rais William Ruto amekashifu matamshi ya Sudi na Ng’eno kupitia Twitter. Lakini hiyo haitoshi, tunamtaka kumwomba Rais msamaha moja kwa moja na kwa njia ya heshima kwa sababu wawili hao ni wandani wake na walitoa matamshi hayo wakimtetea,” Bw Koinange, ambaye ni mbunge wa Kiambaa, akasema kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya bunge.
Mwenyekiti huyo alikuwa ameandamana na wanachama wa kamati hiyo; Peter Kaluma (Homa Bay Mjini), Makali Mulu (Kitui ya Kati), Wachira Kabinga (Mwea), Edward Oku Kaunya (Teso Kaskazini) na Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Kisumu katika Bunge la Kitaifa Rosa Buyu.
“Wakenya wote wanafahamu kuwa Mbw Sudi na Ng’eno ni wandani wa Dkt Ruto; na hivyo hana budi ila kuomba msamaha moja kwa moja kwa Rais Kenyatta na familia ya mwanzilishi wa taifa hiyo Hayati Mzee Jomo Kenyatta na wananchi wa Kenya kwa ujumla. Matamshi ya aina hiyo kwa Rais ni dharau kubwa kwa Wakenya ambao walimchagua kwa wadhifa huo,” akasema Bw Mulu.
Bw Buyu alisema ni kinyume cha tamaduni za jamii za Kiafrika kwa mtu yeyote kumtusi mama ya mwenzake, hasa ikiwa watu hao ni viongozi.
“Kumtusi mamake Rais Kenyatta – Mama Ngina Kenyatta – ni sawa na kuwakosea heshima akina mama wa taifa hili, hasa wale ambao walipigania ukombozi wa taifa hili,” akasema Buyu.
Naye Bw Kaluma aliahidi kuwasilisha mswada wa marekebisho ya sheria ya Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa (NCIC) ili kuweka adhabu kali kwa wanasiasa wenye mazoea ya kuchochea chuki na uhasama nchini.
“Inaonekana kuwa adhabu ya sasa kwa kosa hili ni nyepesi na ndio maana wanasiasa kama vile Sudi na Ng’eno wanatoa matamshi ya aina hiyo. Hivi karibuni nitadhamini mswada bungeni utakaoweka adhabu kali kwa wachochezi kama hawa,” akasema.
Wabunge hao walitaka maafisa wa polisi kuwakamata wanasiasa wachochezi ili wasije wakavuruga amani na utulivu nchini kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.