Michezo

Nkana FC kutoka Zambia wamhemea upya kiungo Duke Abuya wa Harambee Stars

September 8th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

MABINGWA wa Ligi Kuu ya Zambia (ZSL), Nkana FC, wamefichua azma ya kuendelea kujivunia zaidi huduma za kiungo wa Harambee Stars, Duke Abuya kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu.

Mkataba wa miezi sita kati ya Abuya na Nkana ulitamatika Juni 2020.

Sogora huyo wa zamani wa Kariobangi Sharks aliingia katika sajili rasmi ya Nkana mnamo Januari 2020 na ushawishi wake ugani ukawa kiini cha waajiri wake kutawazwa mabingwa wa ZSL mwezi uliopita.

Umaarufu ulianza kumwandama Abuya katika ulingo wa soka mwaka jana baada ya kufunga bao katika sare ya 1-1 iliyosajiliwa na Sharks kwenye mechi ya kirafiki iliyowakutanisha na Everton ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ugani MISC Kasarani. Sharks waliibuka hatimaye washindi wa gozi hilo kwa mabao 4-3 kupitia penalti.

Ingawa Nkana walimpokeza kandarasi ya miaka miwili walipomsajili, mkataba huo ulifupishwa baadaye hadi miezi sita pekee.

“Kocha Manfred Chabinga wa Nkana yuko radhi kujivunia zaidi maarifa yangu. Amekuwa akiwasiliana nami mara kwa mara na anaendelea kushawishi wasimamizi kunipa mkataba mpya ambao ni mrefu zaidi,” akasema Abuya katika mahojiano yake na Taifa Leo.

Ingawa hivyo, mwanasoka huyo wa zamani wa GFE 105, alifichua kwamba changamoto kubwa zaidi inayowakabili Nkana ambao ni mabingwa mara 13 wa ZSL, ni uchechefu wa fedha ambao umekuwa ukishuhudia mishahara ya wachezaji ikicheleweshwa mara kwa mara.

Mbali na Nkana ambao pia wanajivunia huduma za Wakenya Harun Shakava na Duncan Otieno, klabu nyinginezo zinazomvizia Abuya katika ZSL ni Red Arrows na Green Eagles.

“Zipo klabu sita zinazohemea huduma zangu. Kati ya hizo, tatu ni za Zambia, moja ni ya Angola na mbili ni za Afrika Kusini,” akasema Abuya.