Mzee atibua harusi akidai maharusi ni watoto wake
Na STEPHEN ODUOR
WAPENZI wawili waliokuwa tayari kufunga ndoa katika eneobunge la Bura, Kaunti ya Tana River walilazimika kusitisha harusi yao baada ya mwanamume kujitokeza ghafla harusini akidai yeye ni baba yao.
Anne Magwi na Jotham Munini, watoto waliolelewa na wazazi wa kambo, walikuwa wamefika kanisani Jumamosi kwa ajili ya harusi yao.
Kabla wafunganishwe pingu za maisha, mzee mmoja alitokeza na dada zake kusimamisha harusi hiyo wakidai ilikuwa mwiko kwa mwanamume kumwoa dadake.
Kulingana na mchungaji Festus Muli wa Kanisa la Holy Redemption Ministries, mwanamume huyo alidai alikuwa ametengana na mama za wawili hao zamani.
“Alieleza kuwa, alimzaa mtoto wa kiume katika mapenzi haramu na mwanamke mmoja, ambapo uhusiano wao haukuendelea, ilhali mtoto wa kike alikuwa tunda la uhusiano wake na ‘mpango wa kando’,” alisema kasisi huyo.
Mchungaji alielezea kwamba, mwanamume huyo alidai kuachana na mamake Jotham ilipofichuka alikuwa na uhusiano wa pembeni na mwanamke mwingine. Wakati huo mtoto alikuwa na umri wa mwaka mmoja.
Hapo ndipo alipoamua kujenga mahusiano na mpango wa kando, uhusiano ulioshindwa kustahimili mawimbi ya ufukara na kumfanya mwanamke kutoroka akiwa na mimba ya miezi minne.
Anne, ambaye ndio tunda la uhusiano huo alilelewa na baba mwingine kwani mamake aliolewa mwaka mmoja baadaye na mwalimu.
Mchungaji Muli alielezea Taifa Leo kwamba, mwanamume huyo aliwaonyesha picha za wawili hao walipokuwa wadogo, ambazo alizipata kutoka kwa marafiki na jamaa waliokuwa wakiwasiliana naye.
“Ni mtu na familia yake. Alipata ujumbe kutoka kwa rafiki zake ambao pia waliona ujumbe huo ukisambaa katika mitandao ya WhatsApp,” alieleza mchungaji huyo.
Kulingana na mpwa wa mwanamume huyo ambaye hakutaka kutajwa jina, mtu huyo amekuwa akiwatafuta watoto wake kwa miaka 10 bila mafanikio.
Jitihada zake kufikia marafiki wa mke wa kwanza hazikuzaa matunda. Aliarifiwa kupitia marafiki kwamba, mwanamke huyo alikuwa amemzaa msichana anayefanana naye.
“Alimwona binti huyo mara moja katika shule ambayo watoto wake wanasoma. Alionyeshwa lakini hakujua jinsi ya kumfuata amweleze kwani baba mlezi alikuwa amekwenda kumtembelea wakati ule, hakumwona tena baada ya KCPE,” alisema.
Mchungaji Muli alibaini kwamba, ilibidi asitishe harusi na kuwaita wazazi kwenye chumba cha faragha kwa mazungumzo.
Ilibainika kuwa mamake Bwana Harusi alimwarifu kuwa babake alikufa katika ajali ya barabarani akiwa mchanga sana, ilhali msichana huyo alifahamu kuwa babake aliyemlea ndiye baba mzazi.
“Wanawake hawakukanusha kuwa wanamjua mwanamume huyo, na wala hawakukanusha kuwa alikuwa baba yao. Ilikuwa hali ya kusikitisha ila ilibidi tukae chini kusawazisha mambo,” alielezea.