• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 11:13 AM
KINA CHA FIKIRA: Mwerevu hajinyoi, usitumie matatizo unayopitia kulaghai

KINA CHA FIKIRA: Mwerevu hajinyoi, usitumie matatizo unayopitia kulaghai

Na WALLAH BIN WALLAH

MATATIZO yanapoongezeka maishani watu hutumia mbinu nyingi ili waishi.

Wengine hutumia ujanja, utapeli na ulaghai bila kujua kwamba ujanja wa nyani huishia jangwani; ndege mjanja hunaswa na tundu bovu.

Na njia ya mwongo ni fupi!

Bwana Majanga aliachishwa kazi wakati janga la corona lilizuka nchini. Maisha yakawa magumu kwake na familia, watoto wawili na mkewe!

Alipolemewa zaidi, aliamua kuliuza gari lake alilokuwa akilitumia kuenda kazini. Lakini hakupata mnunuzi. Ikambidi aende kwa rafiki yake, Bwana Janja aliyemiliki dukakuu maarufu mjini Mapepe akaombe mkopo. Alimpata Janja ofisini dukani kwake.

Bwana Majanga alimwambia, “Rafiki yangu Janja, tafadhali unikopeshe shilingi elfu tisini, nikachukue bidhaa zangu kutoka Dubai kule bandarini Mombasa. Nitakapoziuza nitapata takribani shilingi milioni nne! Nitakulipa mara moja!”

Bwana Janja alisema, “Shilingi elfu tisini ni nyingi. Lakini ukiwa una kitu cha thamani unachoweza kuweka rehani kama gari, shamba au nyumba, ili ukishindwa kunilipa tuuze unilipe, nitakukopesha!”

Majanga alikubali kuliweka gari lake rehani. Wakakubaliana alipeleke nyumbani kwa Janja saa mbili usiku Janja akishatoka dukani.

Bwana Majanga aliliendesha gari akalipeleka kwa Janja. Alikaribishwa! Wakaingia chumbani. Bwana Janja alitoa pesa akaweka mezani wakazihesabu. Akamshauri Majanga waandikiane karatasi au hati, watie saini kuthibitisha amempa pesa, naye Majanga amemwachia gari rehani!

Lakini Majanga alikataa akasema, “Ndugu Janja, tuaminiane tu! Mimi nikishapata pesa nitakurudishia zako mara moja!”

Majanga aliingiza pesa mfukoni akaondoka bila kuonekana popote tena!

Siku ya nane ndipo Majanga alipoonekana Hotelini Makeke akinywa na kula nyamachoma kuanzia alasiri mpaka saa mbili usiku alipoambiwa alipie bili ya shilingi elfu ishirini hoteli ifungwe! Majanga alidai kuwa pesa aliacha ndani ya gari lake kwenye maegesho ya hotelini nje. Majanga alipelekwa na mlinzi wa hotelini akachukue pesa garini. Alikuwa na funguo za gari mkononi.

Walipofika maegeshoni Majanga alitazama kila upande akalia, “Gari langu halipooo!! Limeibwaaa!!” Polisi waliitwa! Majanga alishtakiwa kwa kosa la kula na kunywa hotelini bila pesa! Polisi waliendelea na uchunguzi kuhusu madai ya gari kuibwa maegeshoni! Siku tano baadaye polisi walilipata gari nyumbani kwa Janja. Majanga alidai kwamba Janja ndiye aliyemwibia gari maegeshoni hotelini. Wakati Janja alijitetea mahakamani, alitoa video iliyoonyesha picha na mazungumzo yote kuanzia dukani mpaka nyumbani Majanga alipolileta gari akachukua pesa akaenda!

Ndugu wapenzi, tusiyatumie matatizo kufanya ujanja, ufisadi na wizi wa pesa za watu au za umma ama za serikali! Matatizo hutatuliwa kwa busara ili watu wapate nafuu! Usijifanye mwerevu! Hata mwerevu hajinyoi! UTAJUTA!

You can share this post!

Corona inaongeza pengo kielimu kati ya watu maskini na...

NDIVYO SIVYO: Tafsiri ya Kiingereza ya ‘it doesn’t...