• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
WANGARI: Wasichana kutoka familia za kipato cha chini wapewe sodo hata wakati shule zimefungwa

WANGARI: Wasichana kutoka familia za kipato cha chini wapewe sodo hata wakati shule zimefungwa

Na MARY WANGARI

KATIKA kipindi cha miezi michache iliyopita, kumekuwa na ripoti za kuhofisha kuhusu kuongezeka kwa visa vya mimba za mapema miongoni mwa wasichana.

Hali hiyo imekuwa ngumu hata zaidi kutokana na changamoto zinazowakabili wasichana wa umri mdogo kuhusiana na siku zao za hedhi hasa wakati huu watoto wangali nyumbani baada ya shule kufungwa.

Hali imekuwa ngumu kiasi kwamba, baadhi ya wasichana wameripotiwa kukubali kushiriki ngono ilmradi wapate hela za kununua sodo.

Utafiti uliofanywa majuzi ulibaini kuwa, watoto wa kike na wanawake katika maeneo yenye mapato ya chini waathirika kisaikolojia wakati wa hedhi.

Usafi nyakati za hedhi bado ni changamoto kuu katika mataifa yanayostawi ambapo suala la maji halijatiliwa maanani ipasavyo.

Wanawake na wasichana hulazimika kukwama makwao na kushindwa kutekeleza shughuli za kawaida wakati wa msimu wa hedhi hasa wale wasio na uwezo wa kupata sodo.

Wengine hata hukosa kuhudhuria shule au kukabiliwa na wakati mgumu wakiwa shuleni kwa sababu ya kukosa sodo.

Utafiti unaashiria asilimia 95 ya wasichana aghalabu hukosa kuhudhuria masomo kutokana na suala la hedhi.

Kutokana na takwimu hizo, ni bayana kuwa kuna haja ya kuwa na bidhaa za usafi miongoni mwa wanawake katika nyakati za hedhi, na kwa bei nafuu.

Ukweli ni kuwa, kuwepo kwa bidhaa za kujisitiri wakati wa hedhi kama vile sodo huwa na athari chanya kijamii na huimarisha wanawake na wasichana kielimu na kitaaluma.

Hata hivyo, kupata vifaa hivyo muhimu kumekuwa ndoto kwa wasichana wengi wachanga waliokuwa wakitegemea sodo za bure wakiwa shuleni.

Baadhi ya wasichana wamegeukia ukahaba au kufanya kazi kabla ya kuhitimu umri, huku wengine wakilazimika kutumia vifaa vinavyohatarisha afya yao wakati wa hedhi.Japo serikali imepiga hatua kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa kuhusu Hazina ya Watu (UNPF) katika mradi wa kusambaza sodo kwa wasichana nchini Kenya, ni dhahiri kuwa bado hatujafikia ufanisi kama nchi.

Kulingana na Kipengele cha Sheria kilichofanyiwa marekebisho kuhusu Elimu ya Msingi, serikali ina jukumu la kuhakikisha kila msichana katika shule ya umma anapata sodo za kutosha bila malipo.

Hivyo basi, serikali na wadau husika ni sharti wahakikishe mahitaji ya afya ya uzazi kwa wasichana hasa kuhusiana na nyakati za hedhi yanapewa kipaumbele.

[email protected]

You can share this post!

MATHEKA: Mageuzi yalenga kufanya raia watumwa wa serikali

Maseneta Kwamboka, Mary Seneta wapatikana na hatia