Makala

Familia yashangaa ni kwa msingi gani naibu mwalimu mkuu alifariki kwa sababu ya 'Covid-19'

September 9th, 2020 Kusoma ni dakika: 5

Na MWANGI MUIRURI

MNAMO Julai 31, 2020, Naibu Mwalimu Mkuu wa Shule ya Upili ya Thaara Bw David Muraguri wa Njeri 49, alikuwa ndani ya gari dogo lililokuwa likielekea Nairobi kutoka Murang’a.

Gari hilo lenye usajili KCB 043 V lilikuwa na abiria watatu pamoja na dereva ambapo mwendo wa saa tisa alasiri likiwa karibu na mtaa wa Mbombo katika kiingilio cha shule ya mmiliki binafsi ya Bishop Mahia-ini, lilihusika katika ajali ndogo.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Murang’a Bw Josephat Kinyua, katika hali ya kukwepa kugongana na lingine ana kwa ana, dereva wa gari alimokuwa Bw Muraguri aliliondoa lake kutoka kwa mkondo wa barabara, likaingia kando mwa barabara na kupinduka ndani ya mtaro.

Manusura wote walipelekwa hadi hospitali ya Maragua Level Four ambapo baada ya gangaganga na huduma ya kwanza walibainika kuwa salama na ambapo hawakulazwa.

Huku gari hilo likivutwa hadi kituo cha polisi cha Murang’a, hawa wanne walionusurika ajali hiyo waliagizwa kuripoti katika hospitali hiyo ya Maragua mnamo Agosti 3, 2020, iwapo wangejihisi na changamoto za kiafya kutokana na ajali hiyo.

“Wikendi hiyo hali ya Bw Muraguri ikawa ya shaka. Alianza kuhisi maumivu makali katika viungo na akawa anatapika uchafu uliokuwa na madoa ya damu,” asema dadake mdogo, Bi Jemimah Njeri.

Jumatatu hiyo ya Agosti 3, 2020, Bw Muraguri alirejea katika hospitali hiyo ya Maragua na mbele ya wauguzi, akatapika ule uchafu wa matone ya damu.

“Basi! Sinema ikaanza. Wote waliokuwa karibu waliagizwa wamwondokee Bw Muraguri, wauguzi wakakimbia kuvaa PPE na ikawa rasmi sasa kuna hatari iliyokuwa ishughulikiwe,” asema Bi Njeri.

Madaktari wakisema ni sawa kukubaliana nao jinsi msemo mganga hajigangi usemavyo na katika busara hiyo, Bi Njeri akiwakilisha familia ya Bw Muraguri akiandamana na marafiki kadha walimwondokea mwenzao ndio ashughulikiwe.

“Alilazwa katika wadi moja lakini muda wa saa chache baadaye ambulansi ikaitwa kutoka hospitali kuu ya Murang’a Level Five na akahamishiwa huko akiwa mshukiwa wa ugonjwa wa Covid-19,” asema Bi Njeri.

Kwa mujibu wa afisa msimamizi wa hospitali ya Murang’a Level Five Dkt Leonald Gikera, “mgonjwa huyu aliletwa akiwa na dalili za Covid-19 na ndipo tukampokea kama mshukiwa wa ugonjwa huo na kumweka katika wadi spesheli ya kushughulikia janga hili, wadi hiyo ikiwa ni nambari tano.”

Ni vyema msomaji uzingatie kwamba hadi wakati huu hakuna matokeo ya vipimo kuhusu Covid-19 yametolewa kumhusu Bw Muraguri na pia ukiwa ni mshukiwa wa Covid-19, unafaa kuwekwa karantini wala sio katika wadi ya wagonjwa waliothibitishwa kuambukizwa virusi hivyo.

Hata hivyo, Dkt Gikera anasema kuwa wauguzi walizingatia ripoti iliyoandamana na mgonjwa kutoka hospitali ya Maragua kumpokea kama mshukiwa wa Covid-19.

Katika ripoti hiyo, aongeza, hakukuwa na ripoti kwamba Bw Muraguri alikuwa ametibiwa athari za ajali na kwamba alikuwa amerejea kliniki kama alivyokuwa ameagizwa na wauguzi Maragua siku tatu kabla ya sasa kujipata katika wadi ya Covid-19.

“Tulijaribu juu chini kumshughulikia lakini tukampoteza mnamo Agosti 5, 2020, kumaanisha alikuwa mgonjwa wetu kwa siku ya Jumatatu, Jumannne na akaaga Jumatano,” asema Dkt Gikera.

Bi Njeri anasema kuwa huenda kutapika damu kwa Bw Muraguri kulikuwa ishara ya majeraha ya ndani yaliyokuwa yakivunja damu wala sio ishara ya Covid-19.

Ukistaajabu ya Musa husemwa huenda hujayashuhudia ya Firauni na hitilafu nyingine kuu ni kwamba, hata baada ya Bw Muraguri kusemwa alikuwa ameugua Covid-19 na ndio ugonjwa ulioishia kumuua, hakuna hatua zilichukuliwa kuwasaka waliokuwa wametangamana naye ili nao wakapimwe maambukizi hayo na ikibidi, wawekwe karantini au walazwe watibiwe.

“Kuanzia wale marafiki watatu aliokuwa nao katika gari la ajali, wauguzi waliowashughulikia Maragua baada ya kuletwa kutoka eneo la ajali, Wasamaria wema waliowakimbiza hospitalini, maafisa wa polisi waliovuta gari hilo la ajali—mamia ya wengine wakiwemo mke wake marehemu na watoto wake pamoja na sisi wengine katika familia; hakuna aliyesakamwa akapimwe kuambukizwa Covid-19,” asema Bi Njeri.

Anaongeza kuwa katika jumuia hiyo yote ya waliotangamana na Bw Muraguri “huu muda wote wa zaidi ya siku 30, hakuna ameugua Covid-19 au kuaga dunia katika hali ya kuzua uwezekano kwamba tuliambukizwa naye.”

Dkt Gikera anakubali kuwa hapo kuna hitilafu lakini anaongeza kuwa “maamuzi hufanywa kulingana na hali.”

Afisa msimamizi kitengo cha afya Kaunti ya Murang’a Joseph Mbai alidinda kutoa maoni yake kuhusu kisa hiki ambacho kimekuja kuchambuliwa kama sarakasi ya Covid-19 huku naye mkurugenzi wa huduma za Afya Kaunti hiyo Dkt Winnie Kanyi akisema hakuwa na ufahamu wa kina kuhusu suala hili hivyo basi kutokuwa na uwezo wa kuchangia.

Bi Njeri anafichua kuwa Bw Muraguri alimpigia simu Jumanne ya Agosti 4 akilalamika kuwa hakuwa akipokea matibabu aliyofikiria yalimfaa na akaomba atafutiwe mbinu ya kutolewa kutoka hospitali hiyo na apelekwe katika hospitali ya Nairobi.

“Nilifanya mpango wa kumhamisha baada ya kuhakikishiwa kuweko kwa kiitanda katika hospitali hiyo ya Nairobi lakini wasimamizi wa hospitali ya Murang’a wakakataa kuidhinisha uhamisho huo,” asema.

Dkt Gikera anasema kuwa “wakati huo kulikuwa na makataa ya Wizara ya afya kuhusu uhamisho wa wagonjwa wa Covid-19 hadi Nairobi.”

Bi Njeri anauliza ikiwa basi Bw Muraguri alikuwa mgonjwa mahututi wa Covid-19 aliyeaga dunia baada ya kulala siku mbili katika wadi mbona hakulazwa katika hospitali mpya iliyo na vitanda na mitambo 35 ya wagonjwa mahututi (ICU) ambazo serikali ya Kaunti ya Murang’a imekuwa ikipigia debe katika vyombo vya habari ya jinsi vilijengwa na kupambwa na vifaa katika kipindi cha siku 19 pekee.

Wadi za ICU) zilizojengwa na serikali ya Kaunti ya Murang’a kwa siku 19 pekee. Picha/ Mwangi Muiruri

“Kulazwa ndani ya ICU katika taaluma hii yetu ya utabibu sio maamuzi mwafaka zaidi kwa kuwa wengi hulemewa sana na mikakati ya wadi hizo na ningetaka wengi wajue kwamba wadi za ICU huzua mauti kwa waathiriwa wengi kutokana na mikakati ambayo hutumika. Ni heri wadi nambari tano ambapo tuko na mitambo ya uhakika katika kunusuru maisha kuliko ICU,” asema Dkt Gikera.

Akaaga dunia Bw Muraguri na kuhamishiwa katika mochari ya hospitali hiyo iliyoko umbali wa mita chache tu.

“Mwili wa marehemu kinyume na hali kwamba maiti za Covid-19 huzikwa katika kipindi kifupi iwezekanavyo, ulikaa katika hifadhi hiyo kwa wiki nzima! Tuliambiwa tupange mazishi kwa njia za kawaida. Isitoshe, alichukuliwa kama maiti ya kawaida tu na akazikwa Agosti 11,” asema Bi Njeri.

Dkt Gikera anasema kuwa “mwili ukiwa haujatambuliwa na kuitishwa kwa ajili ya kuenda kuuzika, unaweza ukakaa katika mochari kwa muda,” naye Bi Njeri akihoji: “Tulitambua mwili siku iyo hiyo aloiyoaga dunia na tukawafahamisha kwamba sisi ndio familia kwake halafi iwe namna gani hakukuwa na kumtambua na kutwaa mwili ukazikwe?”

Bi Njeri anafichua kuwa katika mazishi yaliyoandaliwa katika Kaunti ndogo ya Mukurwe-ini Kaunti ya Nyeri, mwendazake alizikwa na maafisa wa kitengo cha afya ambao hawakuwa wamevalia PPE.

Wakati Taifa Leo ilipigia Dkt Gikera simu tukiomba nafasi ya kupekua faili ya matibabu ya mwendazake, ombi ambalo lilikubaliwa, cha kushangaza zaidi ni kwamba fomu ya matokeo ya vipimo vya Covid-19 kumhusu Bw Muraguri kutoka kwa taasisi ya utafiti wa madawa na magonjwa (Kemri) ilikuwa na muhuri wa Oktoba 1, 2020—siku ambayo mwandishi wa Makala haya aliomba nafasi ya kupekua faili hiyo.

Tafakari hili: Bw Muraguri alisemwa kuwa na ishara za Covid-19 mnamo Agosti 3, 2020, akaaga dunia Agosti 5 na akazikwa Agosti 11 lakini matokeo ya vipimo vya Covid-19 kumhusu viko na muhuri wa Oktoba 1, 2020.

Dkt Gikera akajibu kuhusu suala hilo: “Matokeo hutumwa kupitia baruapepe na huenda mtambo wa Kompyuta katika kutoa nakala ulikuwa na hitilafu ya kuweka tarehe.” Hii ni licha ya kuwa muhuri huo umepigwa kwa kutumia mkono wa binadamu…

Hii Oktoba 1, 2020 baada ya Taifa Leo kuonyesha nia ya kufuatilia kisa hiki ndiyo tena tarehe ambayo Waziri wa Afya Mutahi kagwe alipigia Bi Njeri simu akimwomba awe na subira ya kufuatilia kisa hiki.

Bw Kagwe alifuatiliza ombi lake na ujumbe mdogo wa simu ya mkononi ya Bi Njeri uliosoma: “Niwie radhi, poleni. Ninajaribu kusaka majibu kuhusu suala hili kutoka Murang’a.”

Bi Njeri anasema kuwa hakuwa na ufahamiano wowote na Bw Kagwe hivyo basi kushindwa kujua jinsi alivyopata namba yake ya simu ya mkononi.

Bw Kagwe hakujibu swali letu kuhusu suala hili wala hakuchukua simu yetu ya kufuatilia atudokezee jinsi alivyopata nambari ya simu ya Bi Njeri na kwa nini waziri akawa na haja ya kuitaka familia hii ikomeshe juhudi za kusaka majibu.