NGILA: Afrika yote ifuate Somalia kwa Intaneti ya bei nafuu
Na FAUSTINE NGILA
UTAFITI wa hivi punde zaidi kuhusu matumizi ya Intaneti ulibaini kuwa, Somalia ndiyo inaongoza Afrika kwa kutoza ada za chini zaidi za Intaneti ya simu, na nambari saba duniani.
Utafiti huo uliofanywa na shirika la Intaneti la Uingereza la Cable ulionyesha kuwa licha ya nchi hiyo kutambulika mno kwa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, inawagharimu wananchi Sh53 pekee kupata data ya 1GB.
Kenya, ambayo hujigamba kuwa ‘Silicon Savannah’ ya Afrika, iliorodheshwa ya 9 Afrika na 41 duniani, huku wananchi wakilipa Sh112 kwa kila GB ya data.
Afrika Kusini, ambayo inajulikana kuwa na idadi kubwa zaidi Afrika ya raia waliotajirika, imeshangaza kuwatoza wapenzi wa mitandao Sh460 kwa kila GB, huku Nigeria ikilipisha Sh150.
Je, ni kipi bara hili linaweza kujifunza kutoka kwa Somalia? Nchi hiyo ilipata serikali ya kwanza isiyo na misukosuko miaka michache iliyopita, lakini imepiga hatua kuu katika uchumi wa dijitali.
Mwaka 2019 nilipopata ripoti ya unafuu wa data Afrika, Somalia ilikuwa mojawapo ya mataifa yaliyotoza wananchi hela nyingi zaidi kwa Intaneti – Sh662 kwa kila GB.
Lakini katika kipindi cha miezi 12 iliyopita, taifa hilo limegundua uchumi wa usoni utategemea Intaneti na hivyo kushusha bei kwa asilimia 1150.
Afrika yafaa itambue kuwa, ili kupunguza bei ya Intaneti, lazima washikadau wote wahusishwe, serikali na sekta ya kibinafsi, ili kumaliza ukiritimba wa kampuni chache za Intaneti kutoa huduma hiyo.
Somalia kwa sasa ina kampuni 11 za kuuza intaneti ya simu, Kenya ina tatu. Hatuwezi kutarajia kufikia viwango vya juu vya maendeleo ya kisasa ikiwa tutazidi kufungia nje kampuni zinazotaka kuleta ushindani kwenye soko.
Afrika, kinyume na mataifa yaliyostawi kama Ujerumani, Amerika na Uholanzi yanayotoza raia wao zaidi ya Sh200 kwa kila GB, haina uwezo wa kiuchumi wa kuwezesha wananchi kulipia huduma hiyo kwa bei ya juu.
Waafrika wengi wamelemazwa na changamoto zingine kama ukosefu wa maji, uhaba wa chakula, huduma mbovu za kiafya, viwango vya chini vya elimu, na hivyo kuwaambia walipie intaneti pesa nyingi ni kama kuongeza msumari moto kwenye kidonda.
Kwa kuwa visiki hivi vinaweza tu kutatuliwa kupitia suluhu za kisasa zinazotegemea intaneti, ni muhimu serikali za mataifa haya zichukulie suala hili kwa uzito na kuanza kutekeleza mpango wa kupunguza bei hii.
Ingawa Kenya ina kasi ya juu ya intaneti na pia idadi kubwa ya watu wanaotumia huduma hiyo barani, maendeleo katika kubuni suluhu za kidijitali yatawezekana ikiwa bei ya intaneti itapunguzwa.
Hata hivyo, kasi ni muhimu na mataifa yanayoongoza kwa bei ya chini kama Somalia, Sudan, Algeria, Tanzania na Misri yanafaa pia kufanya juhudi za kuongeza kasi ya huduma hii muhimu ili kuwezesha Waafrika kufanya mambo mengi kwa muda mfupi, na hivyo kuinua zao zilizolemazwa na corona.
Mataifa yaliosalia nyuma kama Malawi na Sao Tome yanafaa kusaidiwa, lakini yenyewe mwanzo yawe tayari kukaribisha washindani kutoka mataifa mengine, ili kuondoa aibu ya kutoza watu zaidi ya Sh2,000 kwa kila GB kila siku.