DPP aamuru Ali Korane atiwe mbaroni kwa tuhuma za ufisadi
Na CHARLES WASONGA
MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji ameamuru kukamatwa na kushtakiwa kwa Gavana wa Garissa Ali Korane na maafisa wengine wanne wa serikali kwa wizi wa Sh233 milioni zilizotolewa na Benki ya Dunia kama ruzuku kwa kaunti hiyo.
Kwenye taarifa kupitia akaunti yake rasmi Bw Haji Alhamisi alisema kuwa amekusanya ushahidi wa kutosha kuweza kuhimili kesi dhi ya Gavana Korane na wanne hao.
“Kwa hivyo naamuru kukamatwa na kushtakiwa kwa watano hao wa kosa la kupora fedha za Benki ya Dunia zilizolenga kufadhili miradi ya maendeleo katika Kaunti ya Garissa,” akasema.
Wengine ambao wamekabiliwa na tuhuma hizo ni Afisa Mkuu wa Fedha Ibrahimu Noor, Mkuu wa Hazina ya Kaunti ya Garissa Mohammed Ahmed Abdullahi, Waziri wa Masuala ya Manisipaa Abdi Shale na Mkuu wa Idara ya Uhasibu katika Manisipaa ya Garissa Ahmed Abdullahi Aden.
Bw Haji alisema kuwa watano hao walipora fedha hizo ambazo zililenga kutumika kagharamia ujenzi wa Soko la Quarbey, kuweka lami barabara kadhaa katikati mwa mji wa Garissa na kujenga mabomba ya maji-taka katika mji wa Garissa.
“Badala ya kutumia fedha hizo kwa miradi lengwa, Gavana Korane na wenzake walizielekeza katika akaunti zao za kibinafsi,” akasema DPP Haji.
Bw Korane ndiye Gavana wa hivi punde kukabiliwa na kesi ya ufisadi na matumizi mabaya ya mamlaka. Wengine waliofikishwa mahakamani hivi majuzi kwa tuhuma za ufisadi ni Gavana wa Migori Okoth Obado na mwenzake wa Tharaka Nithi Muthomi Njuki.