Michezo

Rangers wavamia ngome ya Stima na kumtwaa kiungo Salim Hamisi

September 11th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

POSTA Rangers ndicho kikosi cha hivi karibuni zaidi kuvamia ngome ya Western Stima na kumsajili mwanasoka Salim Hamisi.

Stima wamesalia hoi kutokana na uchechefu wa fedha tangu kujiondoa kwa kampuni ya umeme ya Kenya Power iliyokuwa mdhamini wao.

Tukio hilo limechangia wanasoka wengi wa haiba kubwa kukatiza uhusiano wao na Stima ambao kwa sasa wameagana na zaidi ya robo-tatu ya kikosi kilichowachezea msimu uliopita.

Kati ya wachezaji ambao wameondoka kambini mwa kikosi hicho kilicho na makao makuu jijini Kisumu ni Fidel Origa, Edwin Omondi, Stephen Odhiambo, Kennedy Owino, Maurice Ojwang, Abdallah Wankuru na Samuel Njau.

Kusajiliwa kwa Hamisi kunajiri wiki moja pekee baada ya Rangers kukatiza uhusiano na wanasoka wanne wakiwemo Danson Kago, Brian Osumba na chipukizi wa Harambee Stars, Marselous Ingotsi.

Kwingineko, kiungo Chris Owino wa timu ya taifa ya chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20, anatafuta mwajiri mpya baada ya kukatiza uhusiano wake na FC Talanta ya Ligi ya Kitaifa ya Supa (NSL).

“Kandarasi yangu na Talanta ilikatika miezi miwili iliyopita. Ilivyo, sijaona dalili zozote zinazoashiria kwamba kikosi hicho kitarefusha zaidi muda wangu wa kukichezea. Kwa sasa natafuta kikosi kipya cha kukiwajibikia katika soka ya NSL au KPL,” akasema.