Michezo

AK yatafuta chipukizi wa kushiriki riadha zijazo za Dunia

September 11th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

SHIRIKISHO la Riadha la Kenya (AK) limefichua mpango wa kuita kambini chipukizi zaidi kutoka maeneo mbalimbali ya humu nchini kwa minajili ya Riadha zijazo za Dunia kwa watimkaji wasiozidi umri wa miaka 20.

Riadha hizo zitaandaliwa jijini Nairobi kati ya Agosti 17-22, 2021.

Kwa mujibu wa Barnaba Korir ambaye ni mwenyekiti wa kitengo cha makuzi ya wanariadha chipukizi katika AK, hatua hiyo ya kuteua wanariadha wengine inachochewa na ukweli kwamba wengi wa watimkaji waliokuwa wawakilishe Kenya katika Riadha hizo za Dunia zilizoahirishwa mwaka huu watakuwa wamepita umri wa kufanya hivyo kufikia mwakani.

Korir alisema hivyo alipokuwa akitoa msaada wa chakula na fedha kwa wanariadha 14 chipukizi wanaojifua kwa sasa katika kambi ya Kapsait, Elgeyo Marakwet.

“Tutaendelea kutoa msaada kwa chipukizi ambao wameathiriwa pakubwa na janga hili la corona. Hata hivyo, tunatambua kwamba ipo idadi kubwa ya wanariadha waliokuwa wapeperushe bendera ya Kenya mwaka huu ambao kwa sasa hawawezi kushiriki Riadha za Dunia mwakani,” akatanguliza.

AK itapania kuanza upya mchakato wa kuteua watimkaji watakaoitwa kambini kujumuika na wenzao walioteuliwa mwaka huu (ambao bado wanafuzu kushiriki mbio hizo mnamo 2021) kwa minajili ya kujiandaa,” akasema.

Kapsait ni ngome ya wanariadha matata humu nchini, akiwemo mshikilizi wa rekodi ya dunia katika mbio za marathon, Brigid Kosgei ambaye kwa sasa anajiandaa kutifua kivumbi cha London Marathon kwa upande wa wanawake mnamo Oktoba 4, 2020.