Makala

ONYANGO: Masikitiko wanasiasa kuanza ngoma corona ikiumiza raia

September 12th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na LEONARD ONYANGO

SIASA za matusi ambazo zimeanza kuchipuza humu nchini ni ithibati kwamba Wakenya hatujajifunza lolote kutokana na janga la virusi vya corona ambalo limetikisa ulimwengu.

Inasikitisha kuwa Wakenya tungali tunawapigia makofi na kuwashangilia wanasiasa wanaoendeleza siasa za uchochezi na matusi yasiyokuwa na manufaa kwa uchumi na ustawi wa nchi.

Janga la virusi vya corona limedhihirisha wazi kwamba uchumi wa nchi hii ni dhaifu.

Janga la corona limefichua hali mbovu katika sekta ya afya na kuweka wazi kuwa viongozi hawajali wananchi bali wanashughulikia masilahi yao ya kibinafsi.

Ripoti ya hivi karibuni ya Shirika la Takwimu nchini (KNBS) inaonyesha kuwa zaidi ya Wakenya milioni 1.7 walipoteza kazi kati ya Aprili na Agosti mwaka huu.

Janga la corona limeongeza maradufu idadi ya Wakenya wasiokuwa na ajira kutoka asilimia tano hadi asilimia 10.

Itachukua muda mrefu kwa Wakenya hao waliopoteza kazi kupata ajira kutokana na hali ngumu inayokumba biashara za humu nchini.

Janga la corona lilifichua kuwa huduma za afya humu nchini zingali duni. Kwa mfano, ilibainika kuwa hospitali katika kaunti nyingi hazina vitanda vya wagonjwa mahututi. Aidha, imebainika kuwa taifa hili lina uhaba mkubwa wa wahudumu wa afya.

Wizi wa mabilioni ya fedha yaliyotengwa kwa ajili ya kukabiliana na janga la corona ni ithibati tosha kwamba viongozi hawana na haja nasi bali wanajali masilahi yao ya kibinafsi.

Huo ni wito kwa Wakenya kuwa wanafaa kuchagua viongozi wenye maadili mema na wala si wanasiasa wanaojua kutusi wenzao.

Hatutaweza kuangamiza zimwi la ufisadi endapo tutachagua viongozi kwa kuzingatia kabila na ujuzi wao wa kutusi wenzao.

Serikali inafaa kuingilia kati na kuzima siasa za mapema ambazo zinaongeza joto la kisiasa nchini. Badala yake wanasiasa wanafaa kuanzisha juhudi za kuboresha uchumi ambao umezorota kufuatia janga la virusi vya corona.

Wanasiasa wana jukumu la kuelezea Wakenya watafanya nini kuongeza nafasi za ajira, kuboresha huduma za afya na kumaliza ufisadi. Wakati wa siasa za domokaya umeisha.

[email protected]