Michezo

Chemutai kuendea medali ya dhahabu katika Riadha za Dunia kwa Chipukizi wa U-20

September 11th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRS ADUNGO

MWANARIADHA Zena Chemutai yuko tayari kutamba katika Riadha za Dunia kwa Chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 zitakazoandaliwa jijini Nairobi mwakani.

Zena aliambulia nafasi ya nne katika mbio za mita 3,000 katika makala yaliyopita ya Riadha za Dunia kwa Chipukizi zilizofanyika jijini Tampere, Finland mnamo 2018. Kenya iliibuka ya kwanza mwishoni mwa mashindano hayo.

Bingwa huyo wa Afrika katika mbio za chipukizi wasiozidi umri wa miaka 18 amesema kubwa zaidi katika maazimio yake ni kutia kibindoni nishani ya dhahabu katika mashindano ya mwaka ujao

“Nimekuwa nikijiandaa kwa mbio zijazo za U-20 na nahisi kwamba niko katika hali shwari itakayoniwezesha kuwika katika mashindano hayo,” akasema Chemutai kwa kukiri kwamba ratiba yake ya mazoezi chini ya uelekezi wa kocha Erick Kimaiyo, haijavurugwa sana na janga la corona.

Chemutai amekiri kwamba kujifanyia mazoezi hapo awali kulikuwa jambo zito hadi Kimaiyo alipomwalika kambini kujifua kwa pamoja na wanariadha wengine kwa kuzingatia kanuni zote za Wizara ya Afya katika juhudi za kukabiliana na virusi vya corona.

Chemutai ambaye ni mwanafunzi wa zamani wa Shule ya Msingi ya Keringet Boarding, aliwakilisha Kenya katika Raidha za Dunia za U-20 kwa mara ya kwanza mnamo 2018 ila akakosa kusajili matokeo ya kuridhisha.

Ingawa hivyo, alijiimarisha na akaibuka bingwa wa Afrika katika mbio za mita 3,000 kwenye Raidha za Bara la Afrika baadaye 2018.

“Nimekuwa nikishiriki mazoezi na wanariadha wenzangu kwa minajili ya kivumbi kijacho cha Riadha za Dunia za U-20 na nahisi kwamba nimeimarika kwa kuwa kasi yangu imeboreka,” akasema.

Miongoni mwa wanariadha ambao hufanya mazoezi ya pamoja na Chemutai ni Winnie Kimutai aliyeunga timu ya taifa iliyotarajiwa kuwakilisha Kenya kwenye Mbio za Nyika barani Afrika jijini Lome, Togo mnamo Aprili 2020. Kivumbi hicho kiliahirishwa kwa sababu ya janga la corona.