• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 9:55 AM
Naomi Osaka atandika Azarenka na kunyakua taji la US Open

Naomi Osaka atandika Azarenka na kunyakua taji la US Open

Na MASHIRIKA

NAOMI Osaka, 22, alidhihirisha ubabe wake katika mchezo wa tenisi kwa kujinyanyua na kumkomoa Victoria Azarenka (1-6, 6-3, 6-3) katika kivumbi cha US Open usiku wa Septemba 12, 2020.

Ushindi huo ulimpa Osaka ambaye ni raia wa Japan taji lake la tatu la Grand Slam na la pili kwenye mashindano ya US Open.

Osaka alizidiwa maarifa katika seti ya kwanza na akajipata chini ya pointi 3-0 mwanzoni mwa seti ya pili. Hata hivyo, alijinyanyua na kutawala raundi 10 kati ya 12 zilizofuatia.

Hiyo ilikuwa fainali ya kwanza kwa Azarenka, 31, kushiriki tangu 2013. Nyota huyo raia wa Belarus alishindwa kudhibiti ukali wa mipakuo ya Osaka aliyemvurumishia fataki nzito nzito kuanzia mwanzo wa seti mbili za mwisho.

Ilikuwa fahari, tija na furaha tele kwa Osaka aliyejinyoosha sakafuni kichalichali na kutazama mawingu ya jiji la New York kwa muda baada ya kuibuka mshindi wa mchuano huo.

Ushindi huo uliendeleza rekodi nzuri ya Osaka ambaye kwa sasa ametawala fainali zote za Grand Slam alizozishiriki. Awali, mwanatenisi huyo alikuwa ameibuka malkia wa US Open mnamo 2018 na bingwa wa Australian Open mnamo 2019.

“Sitataka tena kukutana nawe kwenye fainali yoyote nyingine ya Grand Slam. Sikufurahia kabisa kucheza nawe katika fainali. Ulikuwa mshindani mgumu sana na mechi ikaonekana kuwa nzito zaidi kwangu mwanzoni mwa seti ya kwanza,” Osaka akamtania Azarenka.

“Ilikuwa fahari kubwa kuchuana na Azarenka, mwanatenisi mzoefu niliyekuwa nikimtazama akitamba ulingoni wakati nikiwa mtoto. Nilijifunza mengi kutoka kwake wakati huo na nimejifunza mengi zaidi katika fainali hii,” akaongeza Osaka.

Ufanisi wa Osaka dhidi ya Azarenka sasa unamkweza hadi nafasi ya tatu kwenye orodha ya Shirikisho la Tenisi la Duniani (WTA).

Tangu aibuke mshindi wa Australian Open mnamo 2013, Azarenka aliyekuwa akiwania taji lake la kwanza la Grand Slam, alichukuwa likizo ya uzazi kuanzia Disemba 2016.

Osaka ndiye mwanatenisi wa kwanza mzawa wa bara Asia kuwahi kushikilia nafasi ya kwanza duniani katika tenisi ya mchezaji mmoja kila upande.

Kufikia sasa, anajivunia kutia kibindoni mataji matano ya WTA Tour. Alijinyakulia mataji mawili ya kwanza ya Grand Slam kwa mchezaji mmoja kila upande baada ya kutawala vipute vya US Open na Australian Open mnamo 2018 na 2019 mtawalia. Osaka ndiye mchezaji wa kwanza baada ya Jennifer Capriati mnamo 2001 kufikia mafanikio hayo.

Baba wa Osaka, Leonard Francois, ana usuli nchini Haiti na mamake ni mzawa wa Japan. Hata hivyo, Osaka aliishi na kukulia nchini Amerika alikopokezwa malezi ya tenisi tangu akiwa na umri wa miaka mitatu.

Mbali na babake Francois, Osaka amenolewa na makocha stadi zaidi katika ulingo wa tenisi wakiwemo Harold Solomon, David Taylor, Jermaine Jenkins na Sascha Bajin aliyemwongoza kuwaangusha miamba Serena Williams, Victoria Azarenka na Caroline Wozniacki.

Mkufunzi wake wa sasa ni Wim Fissette.

Umaarufu ulianza kumwandama Osaka akiwa na umri wa miaka 16 alipombwaga aliyekuwa bingwa mtetezi wa WTA Tour, Samantha Jane Stour wa Australia katika kivumbi cha Stanford Classic mnamo 2014.

Miaka miwili baadaye, alitinga fainali ya WTA kwa mara ya kwanza na kutamalaki kipute cha Pan Pacific Open 2016. Ushindi huo ulimweka ndani ya orodha ya wanatenisi 50-bora kwenye msimamo wa WTA.

Alitikisa dunia mnamo 2018 kwa kumlaza bingwa mara 23 wa Grand Slam, Serena, 38, katika fainali ya US Open. Ufanisi huo ulimfanya kuwa Mjapani wa kwanza kuwahi kuibuka mshindi wa Grand Slam kwa mchezaji mmoja kila upande.

Osaka kwa sasa ndiye mwanamichezo wa kike anayevutia zaidi kibiashara duniani. Isitoshe, ndiye mchezaji wa kike anayelipwa mshahara mnono zaidi kimataifa. Anashikilia nafasi ya 29 kati ya wanaspoti wanaodumishwa kwa ujira mkubwa zaidi ulimwenguni na thamani ya mali yake inakadiriwa kufikia Sh3.8 bilioni.

Mnamo Mei 2020, Osaka alikomesha ukiritimba wa miaka minne wa Serena wa kuwa mwanamichezo wa kike anayelipwa vyema zaidi duniani baada kujizolea jumla ya Sh4.3 bilioni. Fedha hizo zilizidi zile alizopata Serena mnamo 2019 kwa takriban Sh161 milioni.

Mnamo Oktoba 2019, Osaka alijinunulia kasri la Sh690 milioni jijini Los Angeles, Amerika. Jumba hilo lilikuwa likimilikiwa na mwanamuziki na mwigizaji maarufu raia wa Amerika, Nicholas Jerry Jonas, 28.

You can share this post!

Yafaa Badi ajumuishwe katika baraza la mawaziri?

Messi achezea Barcelona kwa mara ya kwanza tangu kuhama...