• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:10 PM
Barcelona kuvamia tena ngome ya Liverpool na kutwaa Salah, Wijnaldum

Barcelona kuvamia tena ngome ya Liverpool na kutwaa Salah, Wijnaldum

Na MASHIRIKA

LIVERPOOL sasa wana kibarua kigumu cha kumshawishi nyota wao Mohamed Salah kusalia uwanjani Anfield msimu huu baada ya Barcelona kuanika azma ya kumsajili fowadi huyo matata raia wa Misri.

Kocha mpya wa Barcelona, Ronald Koeman amefichua kwamba Salah ndiye anayeoongoza orodha ya wanasoka wapya wanaowaniwa na miamba hao wa Uhispania.

Ingawa Barcelona walihusishwa hapo awali na washambuliaji Lautaro Martinez (Inter Milan) na Pierre-Emerick Aubameyang (Arsenal), Koeman ameshikilia kwamba usimamizi umepania kumtwaa Salah badala ya Sadio Mane ambaye pia ni fowadi wa Liverpool, ili awe kizibo kamili cha kigogo Luis Suarez.

Suarez ambaye ni mzawa wa Uruguay, alitarajiwa kutua Italia kuvalia jezi za Juventus. Hata hivyo, fowadi huyo wa zamani wa Liverpool anaazimia kupiga abautani na kuyoyomea Atletico Madrid ambao hawajawahi kujaza pengo la Antoine Griezmann aliyeagana nao mwanzoni mwa msimu uliopita na kuelekea Barcelona.

“Koeman ameapa kumsajili Salah na dalili zote zinaashiria kwamba atafaulu kusadikisha Bodi ya Barcelona kufungulia mifereji ya fedha na kumtwaa nyota huyo anayewaniwa pia na Real Madrid. Lengo la Koeman ni kujaza pengo la Suarez,” akasema mwanasoka wa zamani wa Ajax na timu ya taifa ya Uholanzi, Sjaak Swart katika mahojiano yake na gazeti la Mundo Deportivo nchini Uhispania.

Salah amekuwa mhimili na nguzo muhimu katika kampeni za Liverpool katika kipindi cha misimu miwili iliyopita iliyowashuhudia wakitawazwa mabingwa wa Kombe la Dunia, wafalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na washindi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Mbali na Salah, Barcelona wanamhemea pia kiungo Georginio Wijnaldum wa Liverpool ili ajaze nafasi iliyoachwa wazi na Ivan Rakitic wa Croatia aliyejiunga upya na Sevilla ya Uhispania mwanzoni mwa mwezi huu.

Kwa mujibu wa Swart ambaye gazeti la Marca nchini Uhispania limeshikilia kwamba ni msiri na rafiki wa karibu Koeman, Barcelona wanapania kufanya Salah na Griezmann kuwa nguzo za kujisuka upya kuanzia msimu huu kwa kuwa ishara zote zimewaaminisha kuwa fowadi na nahodha Lionel Messi ataagana nao mwishoni mwa muhula huu.

Messi, 33, alichezea Barcelona kwa mara ya kwanza tangu jaribio lake la kuhama ugani Camp Nou kugonga mwamba.

Fowadi na nahodha huyo wa timu ya taifa ya Argentina, aliwajibishwa na Koeman mnamo Jumamosi katika mechi ya kirafiki iliyokutanisha Barcelona na Gimnastic de Tarragona. Barcelona waliofungiwa na Ousmane Dembele, Antoine Griezmann na Philippe Coutinho, walisajili ushindi wa 3-1 katika mchuano.

Messi aliwawasilishia vinara wa Barcelona ombi la kutaka kubanduka ugani Camp Nou mnamo Agosti 2020 ila akaamua kusalia kambini mwa kikosi hicho baada ya Manchester City waliokuwa wakimvizia kutakiwa kuweka mezani Sh89 bilioni kwa minajili ya huduma zake.

Barcelona wamepangiwa kuanza kampeni za Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) mnamo Septemba 27, 2020 dhidi ya Villarreal ugani Camp Nou.

Kwa upande wake, Salah aliwafungia Liverpool mabao matatu katika mchuano wa ufunguzi wa EPL uliowashuhudia wakiwapepeta limbukeni Leeds United 4-3 ugani Anfield mnamo Jumamosi.

Liverpool watarejea ugani kuvaana na Chelsea mwishoni mwa wiki hii ugani Stamford Bridge. Chini ya kocha Frank Lampard, Chelsea ni miongoni mwa vikosi vinavyotarajiwa kuwa tishio kubwa kwa maazimio ya Liverpool ya kutetea ubingwa wa EPL. Chelsea wametumia zaidi ya Sh35 bilioni kujisuka upya kwa minajili ya kampeni za soka ya Uingereza na bara Ulaya muhula huu.

  • Tags

You can share this post!

Salah afunga mabao matatu na kuongoza Liverpool kupepeta...

Raila kutua Kisii, Nyamira ‘kufuta nyayo za...