• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 11:05 AM
Azma ya urais ya Wa Iria yachemsha mbio za urithi Mlima Kenya

Azma ya urais ya Wa Iria yachemsha mbio za urithi Mlima Kenya

Na WANDERI KAMAU

MASWALI yameibuka kuhusu mpango halisi wa kisiasa wa Gavana Mwangi wa Iria wa Murang’a, baada ya kutangaza kwamba atawania urais katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Ingawa Bw Wairia hakutoa tangazo moja kwa moja, hilo lilibainika wiki iliyopita wakati makundi kadhaa ya vijana katika kaunti za Nyeri na Kiambu yalijitokeza na kutangaza kuunga mkono azma yake.

Hatua hiyo imemfanya kuongeza idadi ya magavana ambao wametangaza kuwania urais au nyadhifa nyingine za kitaifa katika uchaguzi ujao.Miongoni mwao ni gavana Alfred Mutua (Machakos), Prof Kivutha Kibwana (Makueni), Wycliffe Oparanya (Kakamega) na Hassan Joho (Mombasa).

Bw Wairia anahusishwa na chama cha The Civic Renewal Party (CRP), ambacho ni miongoni mwa vyama vipya vya kisiasa vinavyoendelea kuchipuka katika ukanda wa Mlima Kenya.

Kwa mujibu wa wadadisi wa siasa za Mlima Kenya, upekee wa tangazo la Bw Wairia ni kuwa kinyume na magavana wengine eneo hilo, yeye hajaonyesha kikamilifu mwegemeo wowote kisiasa tangu 2013, licha ya kuchaguliwa kwa tiketi ya Chama cha Jubilee (JP).

Wadadisi wanamwona kama mwanasiasa huru ambaye amejijengea himaya yake kisiasa, “hivyo mienendo yake inapaswa kutazamwa kwa makini.”

“Bw Wairia amejitokeza kuwa mwanasiasa mwenye maamuzi huru. Amejijenga bila kutumia jina la kigogo yeyote wa siasa nchini. Hili ndilo linalofanya tangazo lake kuibua hisia mseto,” asema Bw Geoffrey Munyui, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Katika chaguzi za 2013 na 2017, wanasiasa wengi katika ukanda huo walitumia jina la Rais Uhuru Kenyatta kujijengea umaarufu miongoni mwa wafuasi wao.

Kabla ya kushinda ugavana katika kaunti hiyo, Bw Wairia alihudumu kama mwenyekiti wa Shirika la Kununua Maziwa Kenya (KCC), alikosifiwa sana kwa kuimarisha mapato ya wakulima.Akiwa gavana, amesifiwa sana kutokana na utendakazi wake, hasa katika sekta ya kilimo.

Suala jingine kumhusu ni chanzo cha msukumo wake ilhali hadi sasa, Rais Kenyatta bado hajatoa mwelekeo kuhusu mustakabali wa eneo hilo kisiasa baada yake kustaafu ifikapo 2022.

Baadhi ya wakosoaji wake wanataja uwepo wa “ufadhili kutoka nje” lengo kuu likiwa “kutumiwa kama mradi wa kupinga chaguo litakalofanywa na Rais Kenyatta.”

“Tunafahamu kwamba baadhi ya magavana ambao wameanza kutangaza kuwa watawania urais wanafadhiliwa na viongozi wanaolenga kuvuruga mchakato wa urithi wa Rais Kenyatta ifikapo 2022. Hilo ndilo lengo kuu. Mbona kwanza wasikamilishe mihula yao?” akauliza diwani mmoja eneo hilo ambaye hakutaka kutajwa.

Kwa muda mrefu, kaunti ya Murang’a imekuwa ikionekana kama kitovu cha siasa za uasi katika eneo la Mlima Kenya, hilo pia likitajwa kumsukuma gavana huyo.

“Murang’a ni kaunti ya kipekee ambayo licha ya kuwa na viongozi wengi wanaosifika katika nyanja za kisiasa na kiuchumi, haijakuwa na usemi wa kutosha kuhusu mkondo wa siasa Mlimani na nchini kwa jumla. Nadhani umefika wakati viongozi kama Wa Iria sasa wanataka kumaliza ‘ukimya’ huo,” asema wakili Ndegwa Njiru, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Kaunti hiyo ndiko wanakotoka wanasiasa walioanzisha mfumo wa vyama vingi kama marehemu Stanley Matiba na Charles Rubia.

Vile vile, ndiko wanakotoka baadhi ya mabwanyenye maarufu kama Peter Munga, Chris Kirubi, mwenyekiti wa Benki ya Equity, Dkt James Mwangi, mmiliki wa kampuni ya Royal Media Services (RMS) Samuel Macharia kati ya wengine.Mnamo Jumatano, viongozi na wafanyabiashara maarufu katika kaunti hiyo walifanya kikao maalum katika hoteli moja jijini Nairobi, ambako walijadili kuhusu “mikakati ya kurejesha upya usemi wake katika ulingo wa kitaifa.”

Miongoni mwa wale waliohudhuria ni Mwakilishi wa Wanawake, Bi Sabina Chege, wabunge Mary Waithera (Maragua), Nduati Ngugi (Gatanga), mwanasiasa Peter Kenneth miongoni mwa wengine.Licha ya juhudi hizo, wadadisi wanataja “ukosefu wa sauti moja miongoni mwa viongozi katika eneo hilo” kuwa sababu kuu ya Bw Wairia kujitokeza kutangaza azma yake.

“Viongozi kutoka Murang’a wana ushawishi mkubwa sana nchini. Licha ya ushawishi huo, hawajaonekana kuutumia kuleta sauti zao kwenye siasa za kitaifa kama walivyofanya Matiba, Rubia na Joseph Kamotho,” asema wakili Njiru.

Ili kutoonekana kuendeleza kampeni za mapema, gavana amekuwa akiwatumia mawakala kuvumisha azma yake, hali inayofasiriwa kuwa mbinu ya kutathmini kwa kina mwelekeo wa kisiasa.“Ni mwanasiasa mwenye maono kwani mielekeo ya siasa itazidi kubadilika.

Kuna mengi yatakayoshuhudiwa kabla ya 2022, baadhi yakiwa mchipuko wa vvyama vipya, wagombeaji zaidi na miungano mipya ya kisiasa,” asema Bw Kipkorir Mutai ambaye ni mdadisi wa siasa.Kufikia sasa, duru zinasema kuwa Rais Kenyatta anampendelea Bw Kenneth kuwa mrithi wake, kutokana na juhudi ambazo zimekuwa zikiendelezwa na washirika wa karibu wa rais kama Naibu Mwenyekiti wa Jubilee, Bw David Murathe.

Bw Murathe anasisitiza kuwa Rais Kenyatta ndiye mtu wa pekee atakayetoa mwelekeo wa eneo hilo kisiasa, msimamo unaopingwa vikali na baadhi ya wanasiasa.

You can share this post!

Joho mbishi wa siasa, siku hizi kimya, kunani?

Huyu Mutua ni twiga, amejitokeza ChapChap!