Michezo

Mauro Icardi hususia 'asali' Ufaransa ikipewa kichapo

September 14th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

NA MASHIRIKA

WANDA Nara ambaye ni mkewe mwanasoka Mauro Icardi wa Paris Saint-Germain (PSG), amesema kwamba mfumaji huyo raia wa Argentina hususia kabisa kuchovya asali kila mara miamba hao wa soka ya Ufaransa wanapopoteza mechi.

Hata hivyo, anaamini kwamba tukio la PSG kutinga fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo 2019-20 kwa mara ya kwanza baada ya miaka 27 litawachochea zaidi kuibuka na ushindi katika takriban kila mchuano.

“Najua PSG wataamka baada ya kupoteza fainali ya UEFA muhula jana na mechi ya kwanza ya Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) msimu huu. Watatawaliwa sasa na kiu ya kushinda kila mechi iliyopo mbele yao, na hiyo itanipa shangwe tele chumbani,” akasema Nara ambaye pia ni ajenti wa mumewe katika masuala ya soka.

“PSG jameni msiniangushe tena. Shindeni kila mechi ili nami nipate raha chumbani, kisha nimzalie Icardi watoto wake mwenyewe!” akaandika Nara kwenye mtandao wake wa Instagram.

Katika mahojiano na jarida la La Repubblica Delle Donne nchini Italia wiki jana, Nara, 33, alisema kwamba Icardi hupenda sana kutikisa buyu lake la asali wakisafiri kwenye treni na hufurahia zaidi kutomasa matunda yake mabivu wanapoogelea bwawani.

“Huwa ni raha sana anaporejea nyumbani baada ya PSG au timu ya taifa ya Argentina kushinda mechi. Kilele cha raha hiyo huwa ni bwawani au kupangiwa safari ya ghafla kwenye treni,” akatanguliza.“Huwa hataki hata kuniona wala kunikaribia wanaposhindwa. Hisia zake huzima ghafla!” akasema mwanamitindo huyo aliyefunga pingu za maisha na Icardi mnamo 2014.

Nara alianza kutoka kimapenzi na Icardi mnamo 2013 baada ya kutemana na mwanasoka mwingine mzawa wa Argentina, Maxi Lopez, 36.

Lopez kwa sasa huchezea kikosi cha Crotone nchini Italia.“Niliachana na Lopez kwa sababu alikuwa na jicho kali la nje. Nilirejea Argentina kuwa wakala wa Icardi. Muda haukupita na tukaanza kutoka kimapenzi,” akasema Nara aliyejaliwa watoto watatu katika uhusiano wake wa awali na Lopez – Valentino, Constantino na Benedicto.