Makala

'Changamoto zipo kwa biashara, lakini jipe moyo, faida utaipata'

September 14th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

NA MARGARET MAINA

[email protected]

@maggiemainah

Joyce Wagaki Karanja, 33, alihitimu kutoka Taasisi ya Elimu ya Unahabari ya Afrika Mashariki  na Stashahada ya uandishi wa habari hapo 2014.

“Nilifanya mazoezi yangu katika Royal Media Services, kama mwandishi kwa miezi minne. Nilifanya vizuri, kila mtu alifikiri nilikuwa na sauti bora na hii ilinipa ujasiri mkubwa na nilijua kuwa siku moja nitakuwa kwenye skrini kama mwana habari,” anasema

Lakini hakujua matarajio yake yalikuwa ya muda mfupi. Bi Wagaki anasema kwamba baada ya mafunzo yake alijaribu kuomba kazi katika vituo vyote vya habari lakini jaribio lake la kazi ya ofisi halikuzaa matunda.

“Nilijaribu mkono wangu katika biashara kwa sababu nilihitaji kulipa bili. Safari yangu ya ujasiriamali ilianza na mikoba kadhaa kupitia dadangu, niliuza lakini baada ya muda biashara haikuwa sawa,” anaeleza.

Anakumbuka siku ambayo alitembelea rafiki yake eneo la Eastleigh, jijini Nairobi.

“Rafiki yangu aliniweka nikimngoja na mwishowe hakuja, na kwa sababu nilikuwa nimesikia kwamba Eastleigh ni kubwa ina vitu vizuri tofauti nilidhani ilikuwa ni busara ikiwa ningeondoka mahali hapo na kitu,” alisema.

Na hapo ndipo alijitosa katika biashara ya kuuza marinda aina ya dera.

“Nilinunua dera mbili zangu mwenyewe, nikapiga picha na kuiweka kwenye mitandao ya kijamii “mtu yeyote ambaye angependa hii, anitumie ujumbe, nilipata watu wengi waliotaka kuzinunua,” alisimulia Taifa Leo Dijitali.

Lakini Bi Wagaki anadai kwamba alihitaji kufanya hesabu za haraka na kuona ni kiasi gani angeziuza ili aweze kupata faida.

“Biashara yangu ilianza vizuri. Mteja wangu mmoja alinipa changamoto na akanishauri nizingatie kuingiza viatu kwenye biashara yangu kwani Dera zitakwenda sawa na viatu aina ya sandali.”

Baadhi ya viatu anavyouza. PICHA/ MAGGY MAINA

Kuuliza karibu na Eastleigh wapi angepata viatu na alielekezwa Kariokor ambapo alifanikiwa kununua aina ya viatu ambavyo alikuwa akivitafuta. Bi Wagaki tena alipiga picha zaidi na kuchapisha kwenye ukurasa wa mitandao ya kijamii – Gaki African Wear.

“Hapo mwanzo nilidhani viatu vilikuwa vya ngozi wakati huo sikujua jinsi ya kutofautisha kati ya ngozi na lexin. Lakini niliuza kwa muda mrefu, hadi nikakutana na mshonaji wa viatu ambaye alinitambulisha kwa ngozi,” anasema.

Kwa Bi Wagaki, ilifika wakati haikuwa tena juu ya muundo huo wa zamani, alikuja na muundo mpya,

“Nilipata msukumo wangu kutoka kwa mtandao; nikaanza kutengeneza bidhaa zaidi za Kiafrika kama kiondo, vito vya mapambo na sanduku la vito. Ninatumia muda mwingi mtandaoni kutafuta maoni zaidi,” anaongeza

Hata hivyo amekabiliana na changamoto kadhaa.

“Nimekabiliana na utapeli mtandaoni, nina wateja ambao hufanya agizo ya bidhaa kisha wanakosa kulipa .Kwa wengine hawawezi kutofautisha kati ya ngozi na lexin, kwa hivyo wakati ninapotuma viatu vya mteja baada ya kupokea, wangekataa kulipa pesa kamili,” anaeleza.

Bi Wagaki anadai kuwa biashara ya mkondoni ni ngumu sana na lazima mtu afanye biashara kwa uangalifu.

Biashara ilikuwa inafanya vizuri sana. Wakati mwingine angeweza kupata wateja ishirini kwa wiki; idadi iliendelea kuongezeka

Bi Wagaki ana wateja wa kimataifa na anatarajia kuwa atasambaza bidhaa zake ulimwenguni.

“Nimehesabu hasara zangu, hii imetokea mara mbili hadi tatu, lakini sasa najua vizuri. Tunapata nyenzo zetu hapa Kenya, kwa vitenge, ninazipata kutoka Tanzania na DR Congo. Mtaji wangu wa kuanzia ulikuwa Sh2,000,” anasema

Anaongeza kuwa uzuri wa biashara yake ni kwamba hakuhitaji mtaji mkubwa kwani alitegemea uuzaji mtandaoni tu,

“Kwenye kurasa zangu za mitandao ya kijamii, maelezo yangu yalikuwa na bado ni ‘zinapatikana kwa agizo’, hii ilinipa muda wa kutengeneza viatu na kupelekwa kwa wakati vinapohitajika,” anasema

Viatu vya shanga vinauzwa Sh1,200 na bila shanga Sh1,000, Viatu vya Loofers Sh 1,500 Kiondo Sh 1,000- Sh15,000 na viatu vya watoto Sh600.

Bi Wagaki anashauri wafanyabiashara wanaotamani kuanza biashara kujitahidi kuanza polepole

“Usisubiri wakati utapata hela nyingi, usiogopo kuwekeza, jipe moyo kwa kuwa biashara nzuri ni ile inachukua muda kukuletea faida ya maaana.”