Siasa

Seneta Langat alia polisi walimjeruhi mgongo

September 14th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

SENETA wa Bomet Christopher Langat Jumatatu alipandwa na hisia mbele ya Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai na Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) George Kinoti alipowasuta maafisa wa polisi kwa kuumiza uti wa mgongo wake.

Alisema aliumizwa mwezi jana alipomatwa nyumbani kwake katika mtaa wa Nyayo, Nairobi ma kusafirishwa hadi Bomet kwa tuhuma za kuwalisha kiapo kundi la vijana 200 wawashambulie jamii jirani ya Wamaasai.

Akiongea mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Haki na Masuala ya Sheria na ile ya Usalama, Dkt Lang’at alisema uti na mgongo wake uliumia kutokana na mwendo wa kasi ambao maafisa hao walikuwa wakiliendesha gari lilikuwa likimsafirisha.

“Hawa watu wanatuua. Nimeratibiwa kufanyiwa upasuaji mwingine baada ya majuma mawili kutokana na majeraha ambayo hawa watu walinisababishia,” akasema Lang’at ambaye alionekana mwenye hisia.

Alisema maafisa hao wa polisi pia walimtisha walipofika Narok wakimwambia hivi: “Unaona Narok kwa mara ya mwisho,”

“Mawakili wangu wanafuatilia suala hili na hawajapata jibu maalum,” Seneta Lang’at akasema

Alisema madai aliyowekelewa yalimwathiri kisaikolojia n ahata kiafya kando na kusababisha uhasama kati ya jamii yake ya Kipsigis na jamii jirani ya Wamaasai..

“Maafisa walionikamata waliniambia kuwa lengo kuu lilikuwa kunizuia kupiga kura. Kitendo kama hicho hakipasi kutokea katika taifa linaloheshimu utawala wa kidemokrasia, “ Bw Lang’at akasema.

Mbw Mutyambai na Kinoti waliwakuwa wamealikwa na kamati hizo mbili kufafanua zaidi kuhusu suala la usalama wa wabunge na maseneta.

Hii ni kufuatia kukamatwa kwa Dkt Lang’at na wenzake Cleophas Malala na Steve Lelengwe mnamo Agosti 17, 2020 kwa kile kilichotajwa ni njama ya kuwazuia kupiga kuhusiana na mjadala kuhusu mfumo wa ugavi wa fedha kwa kaunti.