Vikosi vya Kenya Cup vyafutilia mbali mpango wa kukamilisha msimu wa 2019-20
Na CHRIS ADUNGO
KLABU za raga ya humu nchini zimefutilia mbali mpango wa kukamilishwa kwa kampeni za msimu wa 2019-20 katika Ligi Kuu ya Kenya Cup na Ligi ya Daraja la Kwanza (Championship).
Awali, vikosi hivyo vilishikilia msimamo wa kurejelewa kwa mapambano yote yaliyositishwa kutokana na janga la corona kabla ya msimu mpya wa 2020-21 kung’oa nanga.
Mwenyekiti wa mashindano hayo, Xavier Makuba, sasa amesema klabu za Kenya Cup na Championship zimetupilia mbali mpango huo na zinasubiri utaratibu utakaotolewa na Wizara ya Michezo kabla ya kuanza kinyang’anyiro cha muhula ujao.
“Hatuna muda kabisa. Tumefika Septemba tayari. Taratibu zinatuhitaji kufanyia wachezaji, marefa na maafisa wote wa benchi za kiufundi wa klabu za Kenya Cup na Championship vipimo vya corona,” akatanguliza.
“Hilo ni jambo litakalowanyima wanaraga fursa ya kujifua kwa wiki kadhaa kabla ya msimu mpya kuanza. Imebidi tufutilie mbali mipango yote ya awali na kuelekeza macho kwa msimu mpya ambao tunatazamia kuanza Novemba,” akasema Makuba.
Ungamo la Makuba linamaanisha kwamba hapatakuwepo na mshindi wa Kenya Cup wala Championship katika msimu wa 2019-20. Aidha, hakuna kikosi kitakachopandishwa ngazi wala kuteremshwa daraja kutokana na matokeo ya 2019-20.
Mnamo Juni, Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) lilifutilia mbali msimu mzima wa raga ya humu nchini katika hatua iliyoathiri vipute vyote vya Championship, ligi pana za kitaifa, ligi za madaraja ya chini, Enterprise Cup, Great Rift Valley Cup, Mwamba Cup na National Cirucit.
Hata hivyo, KRU ilipiga abautani mwezi mmoja baadaye na kuunda kamati ya watu sita waliopendekeza kurejelewa kwa kampeni za 2019-20 kabla ya muhula mpya kuanza.
Kamati hiyo ilijumuisha Hillary Itela (mkurugenzi wa ratiba za mechi katika KRU), Moses Ndale na Peris Mukoko (wanachama wa Bodi ya KRU), Makuba (KCB), Philip Jalango (Kabras Sugar) na George Mbaye (Mwamba RFC).
Kwa mujibu wa Oduor Gangla ambaye ni mwenyekiti wa KRU, shirikisho kwa sasa linatayarisha ripoti itakayowasilishwa kwa serikali ikitoa mwongozo kuhusu jinsi ya kurejelewa kwa raga ya humu nchini baada ya kutalii hali mbalimbali.
“KRU itafichua wiki ijayo ratiba ya kujifua kwa timu ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande, Shujaa, kwa minajili ya Olimpiki zijazo jijini Tokyo, Japan na mechi za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia mnamo 2022 jijini Cape Town, Afrika Kusini,” akasema Gangla.
Hadi kusitishwa kwa shughuli zote za michezo humu nchini mnamo Machi 2020, pambano la Enterprise Cup ambalo ndilo kongwe zaidi katika historia ya raga ya Kenya, lilikuwa limetinga hatua ya nusu-fainali.
Mabingwa watetezi Kabras Sugar walikuwa wavaane na Homeboyz huku wanabenki wa KCB wakimenyana na Impala Saracens.
Katika Kenya Cup, Homeboyz walitarajiwa kuchuana na Menengai Oilers ambapo mshindi angejikatia tiketi ya kukabiliana na mabingwa watetezi, KCB kwenye nusu-fainali ya Kenya Cup.
Kabras walitazamiwa kupimana ubabe na mshindi kati ya Impala na Mwamba RFC. Hadi kipute cha Kenya Cup kilipofutiliwa mbali, Kabras RFC walikuwa ikiselelea kileleni kwa alama 74, tatu zaidi mbele ya KCB.
Kwa upande wa KRU Championship, Strathmore Leos waliokuwa hawajapoteza mechi yoyote, walikuwa wakiongoza jedwali kwa alama 76, tisa zaidi kuliko Chuo Kikuu cha Masinde Muliro (MMUST) katika nafasi ya pili.
Leos walikuwa wakutane na mshindi kati ya Northern Suburbs na Chuo Kikuu cha USIU-A katika mojawapo ya nusu-fainali huku MMUST wakipimana ubabe na mshindi kati ya Mean Machine ya Chuo Kikuu cha Nairobi na Egerton Wasps.