• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
Grealish avunja moyo Man-United kwa kurefusha mkataba wake Aston Villa hadi 2025

Grealish avunja moyo Man-United kwa kurefusha mkataba wake Aston Villa hadi 2025

Na MASHIRIKA

NAHODHA wa Aston Villa, Jack Grealish, 25, ametia saini mkataba wa miaka mitano na kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Kiungo huyo raia wa Uingereza alikuwa akihusishwa na uwezekano mkubwa wa kubanduka uwanjani Villa Park na kutua Old Trafford kuvalia jezi za Manchester United.

Grealish amekuwa mwanasoka wa Villa tangu akiwa kinda wa miaka minane. Aliwajibishwa na kikosi hicho kwa mara ya kwanza mnamo 2013-14.

“Hiki ni kikosi changu, najihisi nyumbani zaidi na ninafurahia maisha hapa,” akasema Grealisha wakati akitia saini mkataba mpya.

Grealish ambaye aliwajibishwa kwa mara ya kwanza na timu ya taifa ya Uingereza wiki iliyopita dhidi ya Denmark, sasa atachezea Villa hadi 2025.

“Tunapania kumtumia Grealish kama nguzo ya kukisuka kikosi kipya tutakachokitegemea katika kampeni za misimu kadhaa ijayo. Alikuwa mwepesi kurefusha muda wake kwa sababu anakipenda kikosi hiki,” akasema Afisa Mkuu Mtendaji wa Villa, Christian Purslow.

Villa wamepangia kufungua kampeni zao za EPL msimu huu wa 2020-21 dhidi ya Sheffield United mnamo Septemba 21, 2020 baada ya Grealish kuwa mhimili mkubwa uliowasaidia waajiri wake hao kuponea chupuchupu na kusalia ligini mwishoni mwa msimu wa 2019-20.

Katika msimu huo, aliwajibishwa na Villa katika jumla ya mechi 36 kati ya 38 za EPL na akafunga mabao manane likiwemo moja katika sare ya 1-1 dhidi ya West Ham United katika siku ya mwisho ya kampeni za 2019-20.

TAFSIRI: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Onyango alenga kurejea KPL kwa kishindo

Lampard aitaka Chelsea iwapiku Liverpool na Man City