MATHEKA: Mikutano inavyotamba utadhani corona imeisha
Na BENSON MATHEKA
Kwa muda wa majuma matatu sasa, wanasiasa wamekuwa wakiandaa mikutano ya kisiasa inayohudhuriwa na mamia ya watu ambao wamekuwa wakisongamana kinyume na kanuni za kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.
Hii ni licha ya Wizara ya Afya kuonya kuwa ingawa idadi ya maambukizi imekuwa ikishuka, virusi hivyo havijaangamizwa nchini.
Wanasiasa wamekuwa wakipigana pambaja na kusalimiana kwa mikono. Hawavai barakoa au kushauri wafuasi wao kutosongamana. Ajabu ni kuwa baadhi yao wamekuwa wakihudhuria ibada makanisani ambako kanuni za wizara ya afya zinazingatiwa na kunyima Wakenya wengi fursa ya kuabudu.
Kufuatia kanuni hizo, waumini hawawezi kuhudhuria mikutano ya krusedi na mihadhara ambayo haivutii umati mkubwa kama mikutano ya wanasiasa.
Kanuni hizi zimepokonya Wakenya uhuru wao wa kufurahia burudani vilabuni, wamepigwa marufuku kuandaa hafla za kijamii na matamasha ya aina yoyote yanayohudhuriwa na watu wengi.
Wakijaribu kukiuka kanuni hizo, wanakamatwa na maafisa wa polisi walioagizwa kutekeleza kanuni za kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona. Kinaya ni kwamba ni polisi hao wanaowalinda wanasiasa wanaoandaa mikutano ya kisiasa bila kuwachukulia hatua.
Ni polisi hao wanaotumiwa kuwakamata watu watano au ishirini wakiwapata wakilewa katika baa kwa kisingizio cha kukiuka kanuni za wizara ya afya lakini wanawalinda wanasiasa zaidi ya hamsini wanapokutana katika boma la mmoja wao kujadili siasa na kuburudika.
Ni polisi hao wanaomkamata mtu mmoja akiwa ndani ya gari lake peke yake kwa kutovaa barakoa.
Wakati wanasiasa wanaoandaa mikutano ya hadhara, wahudumu wa matatu wanaendelea kutoza Wakenya nauli ya juu kwa kuagizwa kubeba nusu ya abiria ambayo magari yao yanafaa kubeba kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.
Swali ambalo wataalamu wa wizara ya afya walioweka kanuni hizi wanafaa kujibu Wakenya ni je, kuna virusi vya corona vinavyoambukiza maskini na visivyoambukiza wanasiasa?
Au virusi vinavyopatikana Kenya ni spesheli kwa raia wa kawaida pekee wanaotangamana kwingine isipokuwa kwenye mikutano ya wanasiasa? Itakuwa vigumu kuthibitishia Wakenya kwamba kuna virusi vya corona nchini ikiwa wanasiasa wataendelea na mikutano yao bila baadhi yao kuambukizwa.
Matukio ya wanasiasa yanaonyesha kuwa hakuna haja ya kuendelea kuwekea Wakenya kafyu usiku na kuwanyima starehe na riziki yao, hakuna haja ya kuendelea kufunga shule na kunyima Wakenya utamaduni wao wa kuzika wapendwa wao.
Hakuna haja ya kufanya watu kuteseka kwa madai ya kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona ambavyo viongozi hawaviogopi. Hakuna haja ya kutumia polisi kuhangaisha raia kwa kisingizio cha kukabili janga ambalo ni ndoto kwa viongozi na maafisa wa serikali.
Hakuna haja ya kutumia mabilioni ya pesa kukabili janga ambalo mienendo ya viongozi inaonyesha ni hewa nchini. Najua kuna hatari kubwa kwa sababu virusi hivi vimeua maelfu ya watu kote ulimwenguni na vimeua zaidi ya 600 nchini.
Najua wataalamu wanaotazama kanuni hizo zikiukwa wana wasiwasi mkubwa iwapo maambukizi yatalipuka kwa kiwango kikubwa.