Makala

Je, una maoni gani kuhusu chupi?

September 16th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MISHI GONGO

NI desturi ya wanawake wa jamii nyingi za Kiafrika kuficha nguo zao za ndani – chupi na sidiria – zisionekane na watu wengine.

Inakisiwa kuwa aibu kwa mwanamke kuanika au kutandaza nguo hizo hadharani anapozifua.

Wengi wa wanawake hao wamelelewa kwa misingi kuwa kuanika nguo hizo hadharani ni sawa na kuonyesha uchi wao.

Hivyo wanawake wengi huishia kuanika chupi zao vyooni ama vyumba vya kulala ili kuepuka aibu.

Kulingana na mtafiti wa mila na tamaduni za Kiswahili Bi Hamira Saidi ni utovu wa nidhamu kwa mwanamke kudhihirisha vazi hilo.

“Chupi ya mwanamke inatoa habari nyingi kuhusiana na umbo lake. Kwa kuangalia chupi ya mwanamke mtu anaweza kujua sehemu zake za siri zilivyo ambayo si heshima,” akasema Bi Hamira.

Bi Khadija Juma mwanamke wa miaka 60 eneo la Changamwe alisema kuficha nguo za ndani ni jambo lililoanza jadi na kurithiwa na vizazi vinavyochepuka.

Alisema kuwa ni mwiko kwa mwanamke kuanika chupi zake hadharani.

“Tulipokuwa tukiinukia, kutunza chupi na vitambara ambavyo vilitumika kama sodo, ilikuwa miongoni mwa mafunzo tuliyopewa. Nguo hizo hazikutakiwa kuonekana na watu wengine hasa wanaume hivyo tulilazimika kuzificha,” akasema.

Alisema walipofua nguo hizi walizianika chini ya magodoro,chooni au kwenye matendeguu ya kitanda vyumbani mwao.

Wengi walifanya hivi bila kujua athari za kiafya wanazojiwekea.

Kulingana na daktari wa kushughulikia masuala ya uzazi katika hospitali ya Malindi Najma Khalifa nguo za ndani sawia na nyingine hupaswa kuanikwa sehemu zilizo na jua kali ili kuua viini.

Alisema chupi zinapoanikwa sehemu ambazo hakuna jua la kutosha hubeba vidudu vinavyo sababisha maambukizi katika sehemu za siri.

“Mwanamke anaweza kupata maambukizi katika njia ya mkojo, kufanya fangasi, kuwashwa kwa sehemu za siri na kadhalika ambazo zinaweza kuathiri kizazi,” akasema.

Alieleza kuwa miale ya jua ina uwezo wa kuua viini ambavyo vinaweza kusababisha maambukizi.

Ni nadra kuona chupi za wanawake zimeanikwa nje.

Nguo zinazoanikwa ndani hukosa kukauka vizuri hivyo kunuka uvundo.

Aidha inasemekana kuwa kuanika nguo ndani kunaweza kusababisha mzio kama pumh na mgonjwa mwengine ya kupumua kutokana na kuvuta hewa iliyo na bakteria.