Makala

Mwokaji ambaye makuza ya nchini Kenya na Afrika Kusini yamepanua wigo na mtazamo wake kuhusu maisha

September 17th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MARGARET MAINA

[email protected]

ASAPH Thandolwenkosi Ngwenya, amechanganya damu ya Mkenya na raia wa Afrika Kusini. Yeye hasa ni Mkikuyu na Mshona.

Hivyo ni kweli kwamba ni mzaliwa wa Kenya na pia amelelewa Afrika Kusini.

“Kukua kwangu kulikuwa kwa kupendeza; hasa kulelewa na wazazi kutoka sehemu mbili tofauti za dunia,” anasema.

Yeye huzungumza Kiingereza lakini anajitahidi kujifunza Kiswahili.

Ngwenya anasema kuwa kulelewa katika nchi mbili tofauti kulimfundisha tamaduni tofauti, kukamwezesha kukutana na watu mbalimbali, lakini pia wenye imani na hata mitazamo tofauti.

“Kulelewa hivyo kulinifungua akili kwa kuwa kila jamii ina kanuni, imani na mifumo yake. Lakini unaweza kuamua mafanikio yako bila kujali watu wanafikiri ni kawaida au wanafikiria jinsi mambo yanavyopaswa kufanywa,” anasema Ngwenya.

Mara alipokamilisha elimu ya sekondari ndipo alianza kazi za upishi na uokaji.

“Nilikuwa nimemaliza mitihani yangu ya Cambridge katika shule ya Shah lalji Nangpar katika Kaunti ya Nakuru wakati mama yangu alipendekeza nichukue kozi fupi na kwa hivyo nikaamua kwenda shule ya Valentines Cake House,” anasema.

Kilichoanza kama uraibu wa kujifunza kazi ya uokaji polepole kikakua ambapo alianza kutia zingatio katika kuoka keki na mikate na hatimaye akawa ni miongoni mwa watu stadi katika fani.

Alipojiunga na Chuo Kikuu cha Daystar kusomea shahada ya digrii katika Biashara, aliaacha uokaji japo kwa muda.

“Lakini siku zote nilifikiria juu ya kuoka, kama mwanafunzi kila wakati unafikiria njia za kupata pesa, matumizi bora zaidi ya pesa bila ubadhirifu na jinsi ya kujiimarisha kama binadamu,” anafafanua.

Anakiri kuwa kadiri miaka ilivyosonga ndivyo aligundua polepole kuwa hakuumbiwa kazi za kawaida za ofisini na ambazo wengi hutamani.

Keki. Picha/ Margaret Maina

Alikatiza elimu ya shahada baada ya miaka miwili na nusu licha ya kwamba “nilionekana aina ya mwasi machoni mwao.”

Ngwenya alikaa miaka miwili bila kujua jinsi ya kuanzisha biashara.

“Nilikuwa na ovena yangu na vifaa vichache vya kuokea lakini nikawa ninajiuliza nitaanzaje,” anaeleza.

Ukiyavulia sharti uyaoge. Alianza kuoka keki chache tofauti akidhamiria kuziuza mwenyewe, lakini kwa mwaka mzima, aliuza keki moja tu!

Alianza kutumia majukwaa ya mitandao ya kijamii kama nyenzo za kumwezesha kupata wateja. Ni hapo ndipo alianza kupata wateja na idadi yao ikawa inaongezeka kila siku.

“Kupitia mchakato huu nilikuwa najifunza jinsi ya kuuza, jinsi ya kuwasiliana na wateja na jinsi ya kutoa huduma sahihi. Jambo moja ninaloweza kusema ni kwamba mtu yeyote wa biashara lazima aheshimu na kuthamini kila mteja,” anasema.

Keki. Picha/ Margaret Maina

 

Hivi sasa Ngwenya anaoka keki zaidi ya arobaini kwa mwezi na alioka keki zaidi ya mia nne mwaka 2019 na idadi hiyo inaendelea kuongezeka.

“Ndoto yangu ni kuwa na kiwanda cha uokaji na duka la kisasa. Yaani sio duka la keki tu bali pahala ambapo watu wanaweza kuja, kujisikia wakiwa nyumbani na kufurahia bidhaa na vinywaji mbalimbali,” anasema.

Anaongeza: “Lakini wakati huo huo naoka keki mbalimbali kama za kuzaliwa, harusi, maadhimisho ya siku na aina zote za sherehe.”

Keki zake anaziuza kuanzia Sh2,000 kuendelea.

“Ninaamini kwa dhati kuwa kile mtu anaweka akilini ndizo zinazoweza kumsukuma kufanikiwa pamoja na kuwa na uvumilivu, nidhamu na mwelekeo. Mimi huzingatia kufanya kazi kulingana na bajeti ya wateja wangu,” anasema.

Ngwenya pia huwapa watu mafunzo ya uokaji na yeye ni muumini hodari anayeamini kwamba mshumaa haupotezi mwanga wake kwa kuuwasha mwingine.