Makala

Joto jingi Mandera lilivyo na tija kwa wakuzaji tikitimaji

September 17th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

JAPO wakazi wengi wa Mandera ni wafugaji baadhi yao wamekumbatia kilimo kama njia ya kupanua vianzo vyao vya mapato.

Adan Ibrahim ni mmoja wa wakulima ambao wamekodisha sehemu ya shamba kubwa lenye ukubwa wa ekari 94 kando na Mto Daua, linamilikiwa na serikali ya kaunti.

Mkulima huyu anakuza tikiti maji katika kipande hicho cha ardhi ya ukubwa ekari mbili huku wakulima wenzake wakikuza mahindi, vitunguu, papaya miongoni mwa mazao mengine.

Ibrahim anasema aliamua kujishughulisha na kilimo cha tikitimaji baada ya kugundua kuwa yanahitajika kwa wingi jijini Nairobi na miji mingine mikubwa kutokana na ubora.

Husafirishwa kwa ndege na mabasi ya masafa marefu hadi Nairobi ambapo huhifadhiwa katika maghala maalum yaliyoko mtaaa wa Eastleigh kabla ya kuuza wafanyabiashara wa rejareja.“Matikitimaji tunayokuza huku Mandera yanapendwa zaidi na wateja kutoka mbali kwa sababu ya utamu wake.

Hii ni kwa sababu Mandera ni sehemu yenye joto jingi,” Ibrahim anaeleza.“Vile vile, mashamba yetu yana rotuba tosha na hatuhitaji kutumia mbolea za kisasa katika shughuli zetu za kilimo. Hii ndio maana wateja wanapenda mazao yetu ambayo hayana kemikali yoyote,” Ibrahim anaongeza.

Wakulima katika mashamba hayo, yaliyoko umbali wa kilomita mbili kutoka katikati mwa mji wa Mandera huvuta maji kutoka Mto Daua kwa kutumia mitambo waliyopewa na serikali ya kaunti.

“Serikali yetu imetufaa kwa pampu na mifereji ya plastiki ambayo sisi hutumia kuvuta maji kutoka mtoni. Vile vile, idara ya kilimo hutupa mbegu; na yote haya sisi hulipia baada ya kuuza mavuno yetu,” Ibrahim anasema.

Anasema kwa wastani mahitaji hayo yote humgharimu kati ya Sh50,000 na Sh70,000 kwa ekari. Mavuna yakiwa mazuri Ibrahim anaweza kuvuna kati ya tani 30 na tani 40 kutoka kwa ekari la shamba.Kwa kuwa kilo moja ya zao hilo huuzwa kwa hadi Sh30 kwa kilo, wakati hitaji ni kubwa.

Hii ina maana kuwa mkulima huyu huweza kutia kibindoni Sh900,000, kabla ya kuondoa gharama, kutoka kwa ekari moja ya shamba.

Ibrahim anasema kuwa yeye hukuza tikitimaji aina ya “Sukari F 1” kwa sababu ganda lake ni ngumu inapokomaa na huwa haiathiriwi na magonjwa pamoja na wadudu waharibifu.Aina nyingine ya tikitikimaji ambayo hukuzwa eneo hilo ni “Sugar Baby” huhitaji maji mengi na huathirika na magonjwa ikilinganishwa na “Sukari F1”.

Tikitimaji ni tunda lenye manufaa makubwa kwa mwili wa mwanadamu kwani ina vitamin A, C, na B6. Pia ina madini kama vile “Potasisum” na “amino acid”.

Wataalam wa lishe wanasema matunda haya husaidia kupambana na magonjwa sugu kama vile kansa, shinikizo la damu, maradhi ya moyo na yale ya figo. Waziri wa Kilimo, Ufugaji na Uvuvi katika kaunti ya Mandera Mohamed Omar Absiye alisema serikali hiyo huwapiga jeki wakulima kwa kutafutia soko maeneo mbali mbali humu nchini haswa katika miji ya kitalii kama Mombasa.

“Tunawahimiza watu wetu kukoma kutegemea mifugo pekee ambayo nyakati zingine huangamizwa na kiangazi. Wafahamu kwamba kilimo haswa cha mboga na matunda kina faida kubwa zaidi,” Bw Absiye alimwambia mwandishi huyu kwa njia ya simu.