• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
Kundi lililoanzishwa na wanaume kuhakikisha wasichana wanapata sodo

Kundi lililoanzishwa na wanaume kuhakikisha wasichana wanapata sodo

Na WANGU KANURI

HATA ingawa mambo yamebadilika, sio wanaume wote walio na ujasiri wa kuzungumza waziwazi kuhusu hedhi na usafi wa wanawake.

Lakini kuna kundi moja ambalo lilianzishwa na wanaume likiwa na lengo la kuwapa sodo wasichana kila mwaka na hata kuzungumzia suala la usafi wa wanawake bila ya kuona haya.

Mmoja wa wanachama wa kikundi hicho, Caleb Gicheru anatoa maelezo kukihusu na kazi wanayofanya.

Tueleze kwa kifupi kuhusu Share Dignity

CALEB: Share Dignity ilianzishwa mwaka wa 2019 na wanaume watano ambao walikuwa na mtazamo sawa sawa wa kutaka kuwapa wasichana sodo na chupi kila mwaka. Kwa sasa Share Dignity ina jumla ya wanachama zaidi ya 50 ambao ni mchanganyiko wa wanawake na wanaume.

Ni nini kilichochochea kuanzisha Share Dignity?

CALEB: Suala la mtoto wa kike kukosa sodo ni kikwazo kikuu licha ya bidhaa hiyo kuwa kitu cha muhimu kwa kila msichana anapokuwa katika siku zake za hedhi.

Je, nyinyi kama wanaShare Dignity mnajihisi vipi kulizungumzia suala hili waziwazi?

CALEB: Wakati tunaanzisha tukiwa wanaume pekee tuliliangazia suala la hedhi sio kijinsia bali kama suala la utu. Kuwa na hedhi sio jambo la kujionea haya kwa wanawake bali ni jambo la kawaida kwa kila mwanamke duniani. Sisi kama wanaume tuna kina dada, akina mama wazazi, shangazi na hata wake ambao wao huzipata hedhi na kwetu si jambo la kipekee. Kwa hivyo suala la hedhi halifai kukita tu kwa wanawake bali hata kwa kila mwanadamu kwani ni jambo la muhimu kulizungumzia.

Je, nyinyi kama wanaShare Dignity mngewaeleza vipi wanaume wenzenu?

CALEB: Usafi wa wanawake ni kama mada yoyote ile na aliye na hamu ya kufahamu mengi kuhusu mada yoyote huchambua mada hiyo kwenye mitandao ya Google. Kwa mtazamo huo, wanaume wanapaswa kujitosa katika ufahamu wa mada hii ya usafi wa wanawake na hata wao kuchangia katika miradi ya kuelimisha wasichana ambao hawajaanza kupata hedhi na hata wale walioanza, kuwafahamisha kuhusu usafi wao na kuwapokeza sodo. Usafi wa wanawake sio mada ngumu kama vile wengi wa wanaume hufikiri.

Mnakusudia kuwapa wasichana wangapi sodo mwaka huu 2020 ukilinganisha na mwaka 2019?

CALEB: Mwaka huu tunalenga kuwapa wasichana 60 sodo. Idadi hii ni maradufu ya idadi ya wasichana tuliowapa sodo mwaka uliopita. Wasichana hao tunawapa sodo za kila mwezi wa mwaka.

Je, ni nini kinachowatofautisha nyinyi na watu wengine wanaotoa msaada wa aina hii?

CALEB: Hakuna cha kutofautisha mradi wetu na hiyo mingine ila moyo wa kuwapa wasichana sodo ndicho kishawishi kikuu chetu kwani tunaelewa vyema kuwa mradi huu ni mwito wa kusaidia. Isitoshe, ziwa huwepo kwa kuwa chururu za maji hutiririka mle. Kwa hivyo, watu wengi kuelewa kuwa sodo ni kitu cha muhimu, kutasaidia idadi kubwa ya wasichana.

Bila kusahau kuwa kikundi chenu kilianzishwa na wanaume, je nyinyi huhakikisha mmetimiza matakwa yenu bila kuwadhalilisha wasichana kivyovyote?

CALEB: Japo kikundi chetu kilianzishwa na wanaume, tumeweza kuwapata wanawake kadhaa katika timu yetu kwa hivyo tujapoenda kupokeza sodo sisi hufanya hivyo kama tumechanganyika; wanawake kwa wanaume. Hata hivyo, hatuoni haya kulizungumzia suala hili la hedhi kwani tunahakikisha kuwa wasichana tunaowatuza sodo wameelewa kuwa si jambo la kujionea haya bali kuufurahia uwanawake wao.

Je, nyinyi kama wanaShare Dignity mmehakikisha vipi msichana hajakosa kuenda shuleni ama hata kutangamana na wenzake hata akiwa katika siku zake za hedhi?

CALEB: Kwa kumpa kila msichana sodo kiasi cha kila mwezi, mwaka mzima. Hii inahakikisha kuwa msichana yeyote yule aliyepokezwa sodo hakosi kufanya kile anachokuwa akifanya kabla ya siku zake za hedhi.

Mnalenga kufanya mambo gani katika siku za usoni?

CALEB: Sisi kama kikundi tunalenga kupata watu wengi watakaojihusisha na mradi huu na hata zingine ambazo hupokeza wasichana sodo kwani tunaelewa kuwa sodo ni kitu cha muhimu kwa kila msichana kama ilivyo maji kwa mwanadamu. Isitoshe tunanuia kuona kuwa kila msichana nchini hateseki kwa kuwa hana sodo.

Uzoefu wa kuzungumzia hedhi ni jambo ambalo halijakumbatiwa sana. Isitoshe, watu wengi huona haya na hata masomo dhidi yake hudidimia. Je nyinyi kama wanaShare Dignity mnaweza kueleza umma vipi?

CALEB: Tungeeleza umma kuwa wajishughulishe katika ufahamu wa usafi wa wanawake. Kila mtu ana dada, mama, mke na hata shangazi ambaye hangependa aumie kwa kukosa sodo kila wakati yeye huwa katika siku zake za hedhi. Tusiwe wabinafsi wa kutotaka kufahamu changamoto hili linalowakumba wanawake kila mwezi.

You can share this post!

Wachezaji mahiri lakini bado hawajashindia klabu zao taji

ONGAJI: Mashirika yameanika udhaifu wa sekta ya afya Afrika