Hatimaye Thiago Alacantara atua Anfield
Na MASHIRIKA
LIVERPOOL wamejinasia huduma za kiungo Thiago Alcantara wa Bayern Munich kwa kima cha Sh3.8 bilioni.
Alcantara, 29, alijiunga na Bayern kutoka Barcelona ya Uhispania mnamo 2013 na akawa sehemu ya kikosi kilichosaidia miamba hao wa soka ya Ujerumani kukung’uta Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa 1-0 mnamo Agosti 23, 2020 na kutwaa ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).
Kwa mujibu wa magazeti mengi nchini Uingereza, Alcantara atajiunga na kikosi cha Klopp rasmi Ijumaa licha ya kusalia na mwaka mmoja zaidi kwenye mkataba wake wa sasa na Bayern.
Alcantara amekuwa sajili wa pili wa Liverpool muhula huu baada ya mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kumsajili Kostas Tsimikas ambaye ni beki wa kushoto raia wa Ugiriki.
Alcantara alianza kupiga soka yake ya kitaaluma kambini mwa Barcelona na akaanza kuhusishwa pakubwa na Manchester United mnamo 2013 baada ya kocha David Moyes kuaminiwa fursa ya kuwa mrithi wa Sir Alex Ferguson uwanjani Old Trafford.
Ingawa hivyo, uhamisho huo haukufaulu na badala yake akayoyomea Ujerumani kuvalia jezi za Bayern ambao amewahindia mataji saba ya Ligi Kuu ya Bundesliga mfululizo, makombe manne ya German Cup, Kombe la Dunia na ufalme wa UEFA.
TAFSIRI: CHRIS ADUNGO