Draxler aokoa PSG
Na MASHIRIKA
BAO la fowadi Julian Draxler katika dakika za majeruhi lilikomesha rekodi mbaya ya Paris Saint-Germain (PSG) katika mwanzo wa Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) baada ya kuwapiga Metz 1-0 mnamo Septemba 16, 2020.
PSG ambao ni mabingwa watetezi wa Ligue 1, walikuwa wamepoteza mechi mbili za ufunguzi wa msimu huu ligini kwa mara ya kwanza tangu 1984-85 na hadi waliposhuka dimbani kuvaana na Metz, hawakuwa wamepoteza jumla ya mechi tatu mfululizo ligini tangu 2010.
Chini ya kocha Thomas Tuchel, PSG waliokosa huduma za Mbrazil Neymar Jr, walijipata wakiwa na wachezaji 10 pekee uwanjani baada ya Abdou Diallo kuonyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 65 uwanjani Parc des Princes.
Hata hivyo, walilazimika kusubiri hadi dakika ya 93 kufungiwa bao la pekee lililowavunia alama tatu muhimu na Draxler ambaye pia amewahi kuvalia jezi za Schalke 04 na VfL Wolfsburg nchini Ujerumani.
Neymar anatumia marufuku ya mechi mbili baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu kwa pamoja wanasoka wengine wanne kwa kosa la kuzua vurugu mwishoni mwa mechi iliyowakutanisha na Marseille ligini mnamo Septemba 13.
Kutokana na adhabu ambayo Diallo alipokezwa kwa kuvuta jezi la Ibrahima Niane na hivyo kuonyeshwa kadi ya pili ya manjano, PSG kwa sasa wamepokezwa kadi nne za rangi nyekundu kutokana na mechi mbili zilizopita za Ligue 1. Idadi hiyo ya kadi ni ya juu zaidi na inawiana na kadi nyekundu ambazo wanasoka wa miamba hao waliwahi kuonyeshwa kutokana na jumla ya mechi 62 za awali.
PSG ambao walikuwa wenyeji wa mchuano huo, walimkaribisha kikosini kipa Keylor Navas, beki Marquinhos na mshambuliaji Mauro Icardi baada ya watatu hao kuwa miongoni mwa wanasoka saba waliougua ugonjwa wa Covid-19 hivi karibuni kambini mwao.
Ni Angel Di Maria ambaye ni mchezaji wa zamani wa Real Madrid na Manchester United ndiye aliyetamba zaidi katika mchuano huo wa PSG ambao wamepoteza jumla ya mechi tatu mfululizo tangu chombo chao kizamishwe na Bayern Munich kwenye fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Agosti 23 jijini Lisbon, Ureno.
Di Maria alichangia krosi nyingi ambazo vinginevyo, zingezalisha idadi kubwa ya mabao iwapo kipa wa Metz Alexandre Oukidja angekosa kuwa makini langoni mwake.
PSG ambao ni mabingwa mara saba wa taji la Ligue 1 kutokana na misimu minane iliyopita, sasa wanashikilia nafasi ya 15 kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu kutokana na mechi tatu. Alama nne zinatamalaki kati yao na viongozi wa jedwali, Rennes.
TAFSIRI: CHRIS ADUNGO