Arsenal yapata kipa mpya
NA MASHIRIKA
KLABU ya Arsenal imekubaliana na Dijon kusaini kipa Runar Alex Runarsson kutoka timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu nchini Ufaransa.
Kwa mujibu wa tovuti ya Get French Football News, wanabunduki wa Arsenal watachukua kipa huyo mwenye umri wa miaka 25 kwa kima Sh255,769,564.
Ripoti hiyo inasema kuwa raia huyo wa Iceland atasaini kandarasi kuchezea timu hiyo kutoka jijini London kwa miaka mitano.
“Atashiriki vipimo vya afya kwa awamu mbili. Awamu ya kwanza itaanza leo Alhamisi mjini Dijon halafu afanyiwe uchunguzi zaidi wa kiafya mjini Paris,” tovuti hiyo inasema.
Runarsson, ambaye alijiunga na Dijon mnamo Julai 2018, ana kandarasi na klabu hiyo ya Ufaransa hadi Juni 2022.
Hata hivyo, Arsenal imejitosa sokoni kutafuta kipa kuwa kizibo cha raia wa Argentina Emiliano Martinez, 28, ambaye amehamia Aston Villa kwa Sh2.8 bilioni.
Runarsson atashindania nafasi ya kudakia Arsenal mipira dhidi ya Mjerumani Bernd Leno,28, ambaye kwa sasa ndiye kipa nambari moja, Muingereza mwenye asili ya Macedonia Dejan Iliev,25, na Muingereza Matt Macey,26.
Runarsson ni sajili wa tano wa Arsenal katika kipindi hiki cha uhamisho baada ya beki Gabriel Magalhaes na winga wa pembeni kulia Willian. Magalhaes, 22, alitokea Lille kwa Sh3.3 bilioni naye Willian alitua uwanjani Emirates baada ya kandarasi yake na Chelsea kukatika.
Beki Mreno wa pembeni kulia Cedric Soares na beki wa kati Mhispania Pablo Mari, ambao walikuwa Arsenal kwa mkopo msimu uliopita kutoka Southampton na miamba wa Brazil Flamengo, wamenunuliwa kabisa na klabu hiyo.
Arsenal pia imehusishwa na kipa wa Brentford David Raya na viungo Mghana Thomas Partey (Atletico Madrid) na Mfaransa Houssem Aouar (Lyon).
Wanabunduki wa Arsenal wanasemekana pia wanapanga kuuza wachezaji zaidi wakiwemo kiungo mkabaji Lucas Torreira kutoka Uhispania na kiungo wa kati Mfaransa Matteo Guendouzi. Beki wa pembeni kushoto Sead Kolasinac pia amehusishwa na uhamisho hadi Bayer Leverkusen.
TAFSIRI Na GEOFFREY ANENE