• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Vikosi vya raga vyaafikiana hakuna kupanda wala kushuka daraja

Vikosi vya raga vyaafikiana hakuna kupanda wala kushuka daraja

Na CHRIS ADUNGO

VIKOSI vya raga ya Ligi Kuu ya Kenya Cup vimetaka waliokuwa washiriki wote wa kivumbi cha msimu uliofutiliwa mbali wa 2019-20 kusalia vivyo hivyo katika muhula ujao wa 2020-21.

Katika mkutano ulioandaliwa na klabu zote za Kenya Cup, iliafikiwa kwamba msimu mzima wa 2019-20 ufutiliwe mbali baada ya janga la corona kuchangia ugumu wa kukamilishwa kwa kampeni zilizosalia za raga ya humu nchini.

Xavier Makuba ambaye ni mwenyekiti wa vikosi vya Kenya Cup, amesema hapatakuwepo na mshindi wa Ligi Kuu wala Championship katika msimu wa 2019-20.

Ungamo lake linamaanisha kuwa hakuna kikosi kitakachopandishwa ngazi wala kuteremshwa daraja kutokana na matokeo ya msimu uliopita ambao haukukamilika.

“Tumependekeza kwamba vikosi vilivyonogesha kampeni za msimu jana visalie jinsi vilivyokuwa kwa minajili ya muhula mpya ujao,” akasisitiza.

Hatua hiyo itakuwa pigo kwa Mean Machine, Chuo Kikuu cha Masinde Muliro, Chuo Kikuu cha USIU, Northern Suburbs na Strathmore Leos ambao hadi kufutiliwa mbali kwa msimu huu, walikuwa wamefuzu kwa mchujo wa Championship wakilenga kujaza nafasi mbili katika Ligi ya Kuu ya Kenya Cup.

Kwa mujibu wa Makuba, vikosi vitakavyosalia kwenye Kenya Cup katika msimu mpya wa 2020-21 ni Kabras, Homeboyz, Impala Saracens, Mwamba, Menengai Oilers, Nakuru RFC, Nondies, Kenya Harlequins, Blak Blad na mabingwa wa 2018-19, KCB.

Aidha, ni afueni tele kwa Kisumu na Western Bulls zilizokuwa katika hatari ya kuteremshwa ngazi kwenye Kenya Cup mnamo 2019-20. Vikosi hivyo sasa vitakuwa na mwaka mmoja zaidi wa kujaribu bahati yao na kudhihirisha uwezo wao uwanjani kwa mara nyingine.

Kufutiliwa mbali kwa msimu uliopita kunatarajiwa kuchochea Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) kufungua rasmi muhula wa uhamisho wa wachezaji kwa minajili ya msimu mpya.

“Tutarajie KRU itoe idhini kwa vikosi ili vianze kujisuka upya japo baadhi ya klabu tayari zimeanza kujiandaa vilivyo na kusajili wanaraga wapya tayari kwa vibarua vilivyopo mbele,” akaongeza Makuba huku akifichua uwezekano wa msimu mpya wa 2020-21 kuanza Novemba.

Hata hivyo, mkufunzi Mitch Ocholla wa Impala, ametaka msimu ujao wa raga uanze Januari mwaka ujao.

“Zipo taratibu nyingine zinazohitaji kutimizwa ili Wizara ya Afya ikubalie michezo kurejelewa. Mojawapo ni kufanyia wanaraga, marefa na maafisa wote wa benchi za kiufundi wa kila klabu vipimo vya corona. Hili ni zoezi ghali mno kutekeleza. Vyema tusubiri zaidi makali ya corona yapungue ndipo raga irejee kwa vishindo,” akasema Ocholla aliyewahi pia kunoa timu ya taifa ya Shujaa mnamo 2011-12.

  • Tags

You can share this post!

Harambee Stars kupimana nguvu na Chipolopolo

Shule za kibinafsi zaomba msaada