• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Bale kutua Spurs kwa mkopo

Bale kutua Spurs kwa mkopo

Na MASHIRIKA

FOWADI Gareth Bale wa Real Madrid anatazamiwa kutua Uingereza mnamo Septemba 18 kukamilisha uhamisho wake hadi Tottenham Hotspur kwa mkopo.

Kwa mujibu wa magazeti mengi nchini Uhispania na Uingereza, Real na Tottenham zimeafikiana kuhusu uhamisho wa nyota huyo mzawa wa Wales.

Hata hivyo, kocha Jose Mourinho amekana madai hayo kwa kusisitiza kwamba “Hadi nitakapoelezwa kwamba Bale ni mwanasoka wa Tottenham ndipo nitaanza kuzungumza kumhusu.”

“Kwa sasa angali mchezaji wa Real na nahisi kwamba ni muhimu kuheshimu ukweli huo,” akasema mkufunzi huyo raia wa Ureno.

“Siwezi kusema chochote kuhusu mwanasoka wa Real,” akasema Mourinho katika mahojiano yaka na wanahabari mwishoni mwa mechi ya Europa League iliyowakutanisha na Lokomotiv Plovdiv mnamo Septemba 17 nchini Bulgaria.

Mnamo Septemba 17, alishiriki kipindi cha mazoezi kivyake uwanjani Alfredo di Stefano huku akisubiri matokeo ya majadiliano yalikuwa yakiendeshwa na Real na Tottenham.

Beki wa Real, Sergio Reguilon anatazamiwa kukamilisha uhamisho wake hadi Tottenham mnamo Septemba 18. Mhispania huyo mwenye umri wa miaka 23, alichezea Sevilla msimu uliopita kwa mkopo na akawasaidi kunyakua ufalme wa Europa League chini ya kocha Julen Lopetegui.

Bale alijiunga na Tottenham kwa mara ya kwanza mnamo 2007 baada ya kuagana na Southampton. Alisajiliwa na Real mnamo 2013 kwa kima cha Sh11 bilioni. Tangu wakati huo, amefungia Real zaidi ya mabao 100 na akawasaidia kutwaa mataji manne ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Mnamo Julai 2019, Real walitibua mpango wa Bale kuyoyomea China kuvalia jezi za kikosi cha Jiangsu Suning.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Tottenham kuvaana na Shkendija Europa League

Ligi ya Japan yakosa kisa cha corona