• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 1:08 PM
Kariobangi Sharks yasajili mfumaji Douglas Mokaya

Kariobangi Sharks yasajili mfumaji Douglas Mokaya

Na CHRIS ADUNGO 

KLABU ya Kariobangi Sharks imejinasia huduma za fowadi matata wa Nairobi Stima, Douglas Mokaya kwa mkataba wa miaka minne.

Mokaya aliyekuwa tegemeo kuu la Stima katika kampeni za msimu uliopita wa 2019-20 alijipata bila klabu mnamo Julai baada ya waajiri wake kutamatisha mkataba wake. Hatua hiyo ilichangiwa na maamuzi ya kampuni ya umeme ya Kenya Power kusitisha ufadhili wake kwa kikosi hicho.

Mbali na Nairobi Stima, vikosi vingine vilivyoathiriwa na hatua hiyo ya Kenya Power ni Wester Stima kayika Ligi Kuu ya Kenya (KPL) na Coast Stima inayoshiriki Ligi ya Kitaifa ya Supa (NSL).

Hadi kujiunga kwake na Stima, Mokaya alikuwa mwanasoka wa Bidco United. Kusajiliwa kwake na Sharks ni katika juhudi za kikosi hicho cha kocha William Muluya kujaza pengo la fowadi mahiri Harrison Mwendwa aliyeyoyomea kambini mwa mabingwa mara 13 wa KPL, AFC Leopards.

Mwenyekiti wa Sharks, Robert Maoga amesema Mokaya atalazimika kukabiliana ushindani mkali kutoka kwa nyota Patrick Ngunyi, James Mazembe wa Harambee Stars U-23 (Emerging Stars) na Patrick Otieno wa Harambee Stars U-20 (Rising Stars) ili kupata nafasi katika kikosi cha kwanza.

“Tumejitwalia maarifa ya Mokaya kwa mkataba wa miaka minne. Ni mchezaji wa haiba kubwa ambaye ujio wake utaimarisha viwango vya ushindani katika safu ya ushambuliaji,” akasema Maoga.

Mbali na kumsajili Mokaya ambaye alikuwa pia akiviziwa na Leopards kwa kipindi kirefu, Maoga pia amefichua kwamba Sharks wanapania kumtwaa kiungo Vincent Odongo kwa minajili ya kuboresha uthabiti wa safu yao ya kati.

Odongo ambaye ni mwanasoka wa zamani wa Gor Mahia na Western Stima anatarajiwa kujaza pengo la sogora Sven Yidah aliyeyoyomea Nairobi City Stars almaarufu Simba wa Nairobi.

“Kuja kwa Odongo kutarejesha uthabiti katika safu ya kati. Amekuwa katika KPL kwa muda mrefu na analeta tajriba itakayotumivisha zaidi katika kampeni zijazo na pia kuwa kielelezo kwa wanasoka chipukizi kambini mwetu,” akaongeza Maoga kwa kuongeza kwamba Sharks watapandisha ngazi chipukizi zaidi hadi kikosi cha kwanza.

Sharks pia itasajili beki mmoja na kiungo mkabaji watakaojaza nafasi za Amani Kyata na Michael Bodo waliojiunga na Namungo FC na Sofapaka mtawalia.

  • Tags

You can share this post!

Elimu ya vyuoni sasa ni ya mtandaoni – Profesa Waudo

Olunga kucheza dhidi ya Hiroshima