• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 6:45 PM
Bayern wanyeshea Schalke 8-0

Bayern wanyeshea Schalke 8-0

Na MASHIRIKA

SERGE Gnabry alitikisa nyavu mara tatu naye Leroy Sane akafunga bao katika mchuano wake wa kwanza kambini mwa Bayern Munich kwenye gozi la kwanza la msimu huu katika Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) mnamo Septemba 18, 2020.

Mechi hiyo ilikamilika kwa Bayern kuwabebesha wageni wao Schalke 04 jumla ya mabao 8-0 uwanjani Allianz Arena.

Sane, aliyesajiliwa kwa kima cha Sh6.3 bilioni kutoka Manchester City mwishoni mwa msimu uliopita, alichangia pia magoli mawili yaliyofumwa wavuni na Gnabry.

Ushindi huo wa Bayern uliendeleza rekodi nzuri ya Bayern ambao kwa sasa wamesajili ushindi katika jumla ya mechi 22 mfululizo.

Mabao mengine ya Bayern yalijazwa wavuni kupitia kwa Robert Lewandowski, Leon Goretzka, Thomas Muller na chipukizi Jamal Musiala, 17.

Rekodi ya Bayern kwa sasa inaonyesha kwamba wamesajili ushindi kutokana na mechi 30 na kuambulia sare moja pekee katika mashindano yote tangu wazidiwe maarifa mnamo Disemba 7, 2019.

Katika msimu uliopita wa 2019-20, Bayern walitawazwa mabingwa wa mataji matatu; yaani Bundeliga, German Cup na Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Kwa upande wao, Schalke hawajashinda mchuano wowote wa Bundesliga tangu Januari 17, 2020 na wamepoteza jumla ya mechi saba kati ya tisa tangu kurejelewa kwa kampeni za msimu wa 2019-20 mnamo Juni 2020.

Yalikuwa matarajio ya Bayern kushuhudia jumla ya mashabiki 7,500 wakihudhuria mchuano huo wa ufunguzi wa msimu huu ila mpango wao huo ukasitishwa na Meya wa jiji la Munich.

Gnabry alifungua ukurasa wa mabao katika dakika ya nne kabla ya fowadi huyo wa zamani wa Arsenal kucheka na nyavu kwa mara nyingine katika dakika za 47 na 59 mtawalia.

Ushindi wa Bayern ndio mnono zaidi kuwahi kusajiliwa na kikosi chochote cha Bundesliga katika siku ya kwanza ya msimu mpya kwenye Ligi Kuu ya Ujerumani.

Goretzka alifungia Bayern bao la pili kunako dakika ya 19 baada ya kushirikiana vilivyo na Muller ambaye pia alitikisa nyavu katika dakika ya 69 kutokana na krosi ya Robert Lewandowski.

Lewandowski, 32, alifunga mkwaju wa penalti katika dakika ya 31 baada ya kuchezewa visivyo ndani ya kijisanduku.

Mshambuliaji na nahodha huyo wa timu ya taifa ya Poland anajivunia rekodi ya kufunga mabao 55 kutokana na kutokana na mechi 47 za msimu uliopita wa 2019-20.

Bao lililojazwa kimiani na Sane katika dakika ya 71 lilikuwa la kwanza kwa Mjerumani huyo kutia kapuni tangu afungie Man-City katika ushindi wa 2-0 kwenye gozi la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Aprili 2019.

Tineja Musiala aliyewajibishwa na Bayern kwa dakika mbili pekee muhula uliopita, alitokea benchi na kufungia waajiri wake bao la nane. Ufanisi huo unamfanya mwanasoka wa umri mdogo zaidi kuwahi kufunga bao katika historia ya Bundesliga.

Ni mara ya pili kwa Bayern kuwapepeta wapinzani wao kwa kichapo cha mabao manane kwenye mchuano mmoja mwaka huu. Miamba hao wa Ujerumani waliwachabanga Barcelona 8-2 kwenye robo-fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Agosti 15, 2020 jijini Lisbon, Ureno.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Kiongera aahidi makuu kambini mwa Sofapaka

Wataalamu washutumu vyuo vikuu kwa kutoa mafunzo duni