• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 4:10 PM
Oswe astaafu kusakata soka, ateuliwa kuwa meneja msaidizi wa Wazito FC

Oswe astaafu kusakata soka, ateuliwa kuwa meneja msaidizi wa Wazito FC

Na CHRIS ADUNGO

BEKI wa muda mrefu zaidi kambini mwa Wazito FC, David ‘Tiote’ Oswe amestaafu rasmi kwenye ulingo wa usakataji wa soka.

Oswe kwa sasa amepokezwa majukumu ya usimamizi wa kikosi cha mabwanyenye hao. Atakuwa meneja msaidizi wa timu chini ya nahodha wa zamani wa klabu hiyo, Dan Odhiambo.

Kiungo huyo mkabaji amekuwa akivalia jezi za Wazito FC kwa miaka saba iliyopita na alikuwa sehemu muhimu katika juhudi za kupanda ngazi kwa waajiri wake kutoka Ligi ya Kitaifa ya Supa (NSL) hadi Ligi Kuu ya Kenya (KPL) kwa mara ya kwanza mnamo 2017.

“Oswe amekuwa mwaminifu sana kwa klabu kwa kipindi cha miaka mingi. Tumeamua kumpa jukumu la kusimamia kikosi katika benchi ya kiufundi.”

“Hapa Wazito, sisi hutambua na kutuza uaminifu na kwa kujitolea kwake kwa kipindi hicho chote, tumeamua kumpa Oswe majukumu mengine baada ya kuangika daluga zake,” ikasema sehemu ya taarifa iliyotolewa na Afisa Mkuu Mtendaji wa Wazito FC, Dennis Gicheru.

Kwa upande wake, Oswe alisema: “Safari yangu na Wazito FC imekuwa ya kuonewa fahari. Ingawa tumekuwa na nyakati nzuri na za kusikitisha, tulipoteza na kushinda kama timu nzima. Sasa nahisi kwamba muda umefika wa kuondoka ulingoni na kuwapisha chipukizi kuendeleza mambo mazuri tuliyoyaanzisha kambini mwa Wazito.”

Oswe pia alishukuru usimamizi wa Wazito FC kwa kumwaminia nafasi ya kusimamia kikosi na akaahidi kujitahidi vilivyo kutambisha waajiri wake jinsi alivyofanya kwa uaminifu tangu 2013.

“Ningependa kumshukuru Rais wa Wazito, Ricardo Badoer na Afisa Mkuu Mtendaji kwa kuniteua kuwajibikia kikosi katika nafasi hii. Naelewa falsafa ya kikosi na matarajio ya klabu kutoka kwangu,” akasema.

 

 
  • Tags

You can share this post!

Mbunge ataka Uhuru na Raila wamng’oe Ruto

Man-United pua na mdomo kumsajili beki Alex Telles