• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 11:55 AM
Diack atupwa ndani miaka minne kwa ufisadi IAAF

Diack atupwa ndani miaka minne kwa ufisadi IAAF

Na MASHIRIKA

RAIS wa zamani wa Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF), Lamine Diack, 87, amepokezwa kifungo cha miaka minne gerezani kwa hatia ya kushiriki ufisadi.

Raia huyo wa Senegal alikabiliwa pia na mashtaka ya ulanguzi wa fedha, kutumia njia za mkato za kusaidia wanariadha wa Urusi kushiriki matumizi ya pufya na matumizi mabaya ya mamlaka.

Diack alipatikana pia na hatia ya kusaidia wanariadha waliotuhumiwa kutumia dawa za kusisimua misuli na kuwaruhusu kushiriki Michezo ya Olimpiki ya 2012 jijini London, Uingereza.

Kutokana na makosa hayo, alihukumiwa kifungo cha miaka minne gerezani huku miaka miwili katika kifungo hicho ikiahirishwa.

Mawakili wa Diack hata hivyo wameapa kukata rufaa baada ya kusisitiza kwamba hukumu dhidi ya mteja wao “si ya haki, ni ya kinyama na inakiuka haki za binadamu”.

Mbali na kifungo, Diack pia alitozwa faini ya Sh63.9 milioni. Kinara huyo amekuwa akifanyiwa uchunguzi na wajasusi wa Ufaransa kwa miaka minne iliyopita kuhusiana na madai kwamba alipokea hongo ya takriban Sh336 milioni ili kuficha uovu wa kuwepo kwa matumizi ya pufya miongoni mwa wanariadhwa Urusi katika Olimpiki za London 2012.

Jaji aliyeamua kesi yake alisema vitendo vya Diack “vilikiuka maadili ya riadha na vita dhidi ya matumizi ya dawa haramu za kusisimua misuli miongoni mwa wanamichezo”.

Diack alitiwa mbaroni jijini Paris, Ufaransa mnamo Novemba 2015.

Diack aliyedhibiti mikoba ya IAAF kwa miaka 16, alibanduliwa mamlakini mnamo Agosti 2015 na nafasi hiyo kutwaliwa na Mwingereza Lord Coe.

Papa Massata ambaye ni mwanawe Diack alipigwa marufuku ya kutojihusisha kabisa na masuala ya riadha maishani mnamo 2016, alipokezwa kifungo cha miaka mitano gerezani na kutozwa faini ya Sh130 milioni.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Fernandes atawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka 2019-20 kambini...

Villa wamtwaa fowadi Traore kutoka Lyon