Calvert-Lewin afunga matatu na kusaidia Everton kuzamisha West Brom
Na MASHIRIKA
DOMINIC Calvert-Lewin alifunga mabao matatu katika mechi moja kwa mara ya kwanza katika taaluma yake ya usogora na kusaidia Everton kuchabanga limbukeni West Bromwich Albion 5-2 katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ugani Goodison Park mnamo Septemba 19, 2020.
James Rodriguez naye alifunga bao katika mechi hiyo ya kwanza ugani Goodison Park na kuendeleza mwanzo bora wa Everton katika kampeni za EPL msimu huu.
West Brom walijiweka kifua mbele katika dakika ya 10 kupitia kwa bao la Grady Diangana kabla ya Calvert-Lewin kusawazisha mambo kunako dakika ya 31.
Rodriguez alifanya mambo kuwa 2-1 mwishoni mwa kipindi cha kwanza baada ya kushirikiana vilivyo na Richarlson Andrade.
Sekunde chache baadaye, Kieran Gibbs na kocha Slaven Bilic walionyeshwa kadi nyekundu kwa upande wa West Brom baada ya Gibbs kumsukuma Rodriguez naye Bilic kuwafokea maafisa wa mchuano huo.
Licha ya kujipata wakisalia na wanasoka wachache uwanjani, West Brom walisawazishiwa na Matheu Pereira katika dakika ya 47. Hata hivyo, furaha yao haikudumu kwa muda mrefu baada ya Michael Keane kufungia Everton bao la tatu kutokana na mpira wa Richarlson ambao ulipanguliwa na kipa Sam Johnstone katika dakika ya 54.
Calvert-Lewin alifunga mabao yake mengine mawili katika dakika za 62 na 66 baada ya kuandaliwa krosi safi kutoka kwa Rodriguez na Richarlison mtawalia.
Everton wamesajili sasa ushindi katika mechi zao mbili za ufunguzi katika EPL kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka minane. West Brom watasubiri zaidi kupata alama yao ya kwanza katika EPL msimu huu.
Everton wanajivunia ufufuo mkubwa chini ya kocha Carlo Ancelotti na ujio wa sajili wapya Allan na Abdoulaye Doucoure unatarajiwa kuimarisha kabisa uthabiti wa kikosi hicho.
Everton kwa sasa wanajiandaa kusajili ushindi wa nne kutokana na mechi nne za ufunguzi wa msimu huu watakapotua ugani Selhurst Park kuvaana na Crystal Palace mnamo Septemba 26, 2020. Kwa upande wao, West Brom watakuwa wenyeji wa mabingwa wa 2016-17, Chelsea siku hiyo.
TAFSIRI NA : CHRIS ADUNGO