Makala

Hajutii uamuzi wa kuunda juisi na kuuza nafaka

September 20th, 2020 Kusoma ni dakika: 5

Na SAMMY WAWERU

Mapenzi katika upishi yalimuingia Pauline Kinja akiwa angali mdogo kiumri ambapo anasema alianza kupika akiwa shuleni.

Anafichua kwamba alipika chapati, samosa na mandazi kwa mara ya kwanza akiwa na umri wa miaka 15. “Niligundua nimejaaliwa kipaji cha upishi nikiwa mchanga,” Pauline, 40, anasema.

Anaendelea kueleza kwamba alianza kujishirikisha katika shughuli za kupalilia talanta yake. “Baada ya kuhitimu kidato cha nne 1998, wakati wangu mwingi niliutumia katika mapishi ya vyakula tofauti ili kukuza kipaji changu,” anasema.

Hata baada ya kupata mchumba na kuoleka, Pauline anaiambia ‘Taifa Leo’ kwamba hakukunja jamvi shughuli ya mapishi. Anasema aliendelea kuinogesha ambapo mumewe alimpiga jeki.

Kulingana na mama huyo, kwa sababu hakuwa na uwezo kifedha kukodi chumba maalum kama jiko, alikuwa akifanyia upishi wanakoishi.

Kufuatia kuimarika kwa teknolojia, hasa mitandao ya kijamii kama vile Facebook na WhatsApp ilipojiri nchini, Pauline anasema aliitumia kupakia na kuchapisha picha za vyakula alivyoandaa, zilizoandamana na maelezo, hatua anayoisifia kuchangia kupata wateja.

Akiwa mkazi wa mtaa wa Southlands, eneo la Langata, Kaunti ya Nairobi, alitangulia na majirani. “Eneo tunaloishi, majirani tuna kundi la WhatsApp na ambalo nililitumia kutafuta wateja,” adokeza. Changamoto zilizoibuka, anasema ni kujaribu kushawishi wakazi mitaa mbalimbali Lang’ata, kuhusu juhudi zake.

Mpishi huyo anaendelea kueleza kwamba alifugua ukurasa wa mapishi kupitia akaunti yake ya Facebook, Pau delicacies and caterers na kuchapisha huduma zake. “Oda zilianza kumiminika, kiasi cha kushindwa kuhudumia wateja wote,” anakumbuka.

Baadhi ya oda alizopata kuanzia 2017 ni pamoja na hafla za harusi, mikutano na hafla rasmi za viongozi mashuhuri, kati ya nyinginezo, Nairobi, Nakuru, Murang’a na Kiambu. Aidha, huduma zake zilikuwa tamba.

Kilichoanza kama mzaha, kikawa fursa ya kazi katika sekta ya upishi. Mwaka wa 2018, Pauline alikodi chumba cha mapishi, kikawa jikoni. “Kazi iliimarika, kila Jumamosi ratiba yangu ilikuwa kuhudumia wateja, na pia baadhi ya Jumapili,” Pauline anaelezea, akiongeza kwamba nembo yake ‘Pau delicacies and caterers’ aliisajili rasmi kama kampuni ya huduma za mapishi.

Usafirishaji wa vyakula ulikuwa changamoto, na anadokeza kwamba 2019 alinunua lori la shughuli hiyo, kupitia mapato ya upishi.

Ni mafanikio ambayo yaliendelea kunoga hadi 2020, ambapo mwezi Machi Kenya ilithibitisha kuwa mwenyeji wa Homa ya virusi vya corona (Covid-19), janga analosema lilisambaratisha kwa kiasi kikuu jitihada zake.

Pau delicacies and caterers ilikuwa na wafanyakazi 38 wa ziada na 5 wa kila siku. “Mwaliko wa hafla ya mwisho ulikuwa Machi 13, 2020, siku ambayo Kenya iliandikisha kisa cha kwanza cha Covid-19,” Pauline anafichua.

Kufuatia mkurupuko wa corona nchini, serikali ilipiga marufuku maandalizi ya hafla za umma, hatua ambayo imeathiri sekta ya biashara, hoteli na utalii, na uchumi kwa kiasi kikubwa.

Ni ugonjwa anaosema ulisimamisha ghafla biashara iliyokuwa ikimuingizia mapato yasiyopungua Sh400, 000 kwa mwezi. “Sikuwa na budi ila kutii amri ya marufuku ya mikusanyiko ya watu iliyotangazwa, kama mojawapo ya mikakati kuzuia msambao wa corona. Biashara iliyonichukua muda kuiimarisha ikasimama, kwa muda usiojulikana,” anafafanua.

Miezi kadhaa kabla ya Machi 2020, Pauline anasema alikuwa ametoka nchini China kununua vifaa zaidi kuimarisha kazi yake ya upishi, vilivyomgharimu kima cha Sh3 milioni.

“Ilikuwa pigo kubwa, nusra nilemewe na msongo wa mawazo. Wiki ya kwanza niliwaza na kuwazua nitakachofanya kuzimbua riziki,” anasema, akieleza kwamba wiki moja baadaye alianza kutoa mafunzo ya upishi kupitia mitandao.

Akiwa na uzoefu wa miaka kadhaa katika mapishi, Pauline anasema wazo lilimjia, kulisha wakazi eneo analoishi. “Kipindi hiki, watu wanaelekeza mapato yao kununua bidhaa za kula na kukithi mahitaji mengine muhimu ya kimsingi,” anaelezea, akidokeza kuwa aliingilia biashara ya bidhaa mbichi za kula.

Aidha, aligeuza gari lake kuwa duka tamba. Anafafanua kwamba alianza kuchuuza mazao ya kilimo kama vile viazi, kabichi, njegere (maarufu kama minji), matunda, karoti, vitunguu saumu na pia tangawizi, hatua iliyomgharimu mtaji wa Sh70, 000.

Baadaye, Pauline anasema aliimarisha biashara yake, kwa kukodi duka lenye ukubwa wa mita 3 kwa 10, analolipia kodi ya Sh15, 000 kwa mwezi.

Alijumuisha nafaka kama vile; ndengu, maharagwe tofauti, njahi, mchele, njugu, unga unaotokana na nafaka, miongoni mwa bidhaa zingine za kula.

Pauline anaeleza kwamba suala la bidhaa bichi, hususan matunda kuharibika na pia kuoza lilimhangaisha kwani kuna baadhi ya zilikosa kununuliwa hadi kuisha. “Bidhaa kama vile matunda, yanadumu muda mfupi. Sina jokofu maalum kuhifadhi bidhaa bichi. Niliingiwa na wazo la kuyaongeza thamani, na kulikumbatia mara moja, nikaanza kuyageuza kuwa sharubati,” anasema.

Mfanyabiashara huyo hutengeneza juisi ya stroberi, mananasi, karakara, matufaha, ndizi, matundadamu, machungwa na pia ya viazisukari, bila kutumia viungo vyenye kemikali. Badala ya kutia sukari ili kuongeza ladha, hutumia asali.

Pauline ambaye ni mama wa watoto wanne, pia huunda sharubati ya miwa na kutengeneza maziwa ya mtindi maarufu kama Yoghurt. Hutumia viungohai vya tangawizi, ndimu, mint, mbegu za chia zilizopondwapondwa, smoothies na celery.

Duka lake na lililoko eneo la Southlands, mtaa wa Lang’ata ni lenye shughuli chungu nzima.

Katika mojawapo ya kona ya duka hilo, ni kiwanda cha shughuli hiyo ya kutengeneza juisi, chenye ukubwa wa mita 2 upana, na mita 5 urefu.

Vifaa anavyotumia ni vilivyoko kwenye majiko yetu. Vinajumuisha, mashine aina ya blender ambayo Pauline anafichua ilimgharimu Sh25, 000, japo anasema kwa mwanzilishi katika baishara hiyo akiwa na Sh4, 500 atapata bora kusaga matunda.

Kiwanda hicho pia kina mashine aina ya juicer na ya kusaga miwa, maarufu kama cane crasher, jagi na kichujio.

Mjasirimali huyo anasema mradi huo unaomtia tabasamu, ulimgharimu kima cha Sh500, 000 kuuimarisha, kiasi fulani cha pesa hizo akisaidiwa na mumewe.

Wakati wa mahoajino alisema hajutii kamwe kukumbatia mkondo wa kuongeza thamani mazao mbichi ya kilimo.

“Biashara yangu huimarika kila uchao na ni kwa neema ya Mwenyezi Mungu. Kiwango cha wateja kinaendelea kuongezeka, na huenda siku za usoni kiwanda changu cha sharubati kikawa kati ya vile maarufu kutengeneza juisi nchini,” Pauline akasema.

“Wafanyakazi wangu watano niliowaajiri wakati wa shughuli za mapishi nilisalia nao. Wamesomea taaluma za upishi na huduma za mikahawa, na wamekuwa wenye mchango mkubwa kuimarisha biashara ya uundaji juisi,” akaelezea mfanyabiashara huyo.

Alisema mauzo yakiwa bora, kwa siku hakosi kuingiza zaidi ya Sh4, 500, mapato haya yakiwa faida pekee. Bei ya sharubati huuza kati ya Sh40 – 200, kulingana na kipimo.

Anasema mitandao ya Facebook na WhatsApp, imemsaidia kuvumisha mradi wake maarufu kama Palde Groceries.

“Ugonjwa wa Covid-19 umesababisha wengi kupoteza kazi, wengine bwana zao. Hata hivyo, ukiwa na Sh1, 000, una mtaji wa kutosha kuanza kutengeneza maziwa ya mtindi. Yanahitaji maziwa freshi na viungohai pekee. Tangulia na majirani, kama wateja kufungua jamvi sawa na nilivyoanza,” Pauline anashauri.

Ukizuru mengi ya masoko nchini, hutakosa kutazama mazao ya shamba hasa matunda, mboga na viazi, yakiwa yametupwa na kutapakaa.

Kwa Pauline, huo ni utajiri unaotupwa kiholela. “Mazao kama vile matunda yanaweza kuongezwa thamani kwa kuyaunda sharubati,” anasisitiza, akieleza kwamba uongezaji thamani pia huongeza bei ya bidhaa.

Taswira ya masoko si tofauti na ya mashambani, ambapo utaona mazao yametupwa au hata kulishwa mifugo kwa sababu ya ukosefu wa soko.

“Mbali na juisi, kuna baadhi ya matunda na mazao mengine mabichi hutumika ktengeneza divei,” anasema Steven Mwanzia, mkulima wa matunda aina ya bukini.

Sawa na matunda, mboga na viazi, pia zinaweza kuongezwa thamani na kuepusha wakulima na wafanyabiashara dhidi ya kero la mawakala.

Muhimu zaidi kuafikia hayo, ni kufanya hamasisho, kulingana na Roger Wekhomba, ambaye ni mtafiti. “Ustawishaji wa sekta ya viwanda, chini ya mojawapo ya Ajenda Nne Kuu za Rais, utaafikiwa ikiwa serikali itafanya hamasa ya uongezaji mazao ya kilimo thamani,” anasema Roger ambaye pia hutengeneza mafuta ya kujipodoa kwa mazao ya kilimo.

Hatua hiyo, mdau huyo anaeleza kwamba itasaidia kuimarisha sekta ya viwanda nchini, ili kuangazia suala la ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana.

“Shirika la Kutathmini na Kudhibiti Ubora wa Bidhaa Nchini (Kebs), ni kati ya taasisi bora zaidi nchini. Ukiibuka na wazo la kuongeza mazao thamani, wasilisha sampuli kwa Kebs na maafisa wake watakusaidia,” Roger anahimiza.

Huku Pauline Kinja akiwa na matumaini kurejelea katika biashara yake ya mapishi, kufuatia kuonekana kupungua kwa maambukizi ya Covid-19, serikali itakapoondoa marufuku ya mikusanyiko ya watu, anasema ataendelea kuimarisha Palde Groceries.

“Mapishi, uuzaji wa bidhaa za kula na utengenezaji wa juisi, huenda sambamba,” anasema.