• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Polisi watibua kikao cha Khalwale kwa ‘amri kutoka juu’

Polisi watibua kikao cha Khalwale kwa ‘amri kutoka juu’

Na SHABAN MAKOKHA

POLISI katika Kaunti ya Kakamega, Jumapili waliwatawanya wanasiasa kumi wanaoegemea mrengo wa ‘Tangatanga’, waliokuwa kwenye mkutano na wajumbe kutoka wadi sita katika Kaunti Ndogo ya Shinyalu.

Wanasiasa hao walikuwa wakifanya mkutano katika makazi ya mtu aliyetambuliwa kama Bw Lumumba “kujadili masuala yanayoliathiri eneo la Magharibi.”

Viongozi hao walijumuisha aliyekuwa seneta wa Kakamega Boni Khalwale, wabunge saba na madiwani.

Wabunge waliokuwepo ni Ben Washiali (Mumias Mashariki), Mwambu Mabonga (Bumula), Didimus Barasa (Kimilili), Justus Murunga (Matungu), Malulu Injendi (Malava), Charles Gimose (Hamisi), na Dan Wanyama (Webuye Magharibi).

Wabunge wanne walikuwa washahutubu wakati kikosi cha polisi kikiongozwa na Mkuu wa Polisi katika eneo hilo, Bw Robert Makau kilipoingia kwenye makazi hayo kwa nguvu na kuagiza mkutano huo kusimamishwa mara moja wakidai ulikuwa ukikiuka kanuni za corona.

Wanasiasa hao walijitetea vikali, wakisema kuwa idadi ya washiriki ilikuwa chini ya watu 100 lakini polisi hawakusikiliza.

“Tumepewa maagizo kutoka juu kuhakikisha mkutano huu hauendelei. Tunamwagiza kila mmoja kuondoka mara moja,” akaagiza.

Wanasiasa hao waliilaumu serikali kwa maonevu kwenye utekelezaji wa kanuni hizo.

Bw Washiali alishangaa kuhusu sababu ya baadhi ya viongozi kutoka eneo hilo kuruhusiwa kufanya mikutano yao bila kuingiliwa kwa namna yoyote ile huku wao wakizuiwa kujadili masuala yanayowaathiri wakazi.

“Tumemwona Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi (Cotu) Francis Atwoli akiwaalika mamia ya watu nyumbani kwake katika Kaunti ya Kajiado. Mbona sisi tunazuiwa?” akashangaa.

  • Tags

You can share this post!

Wabunge waapa kushinikiza NG-CDF iongezwe

Mashirika yataka Obado aendelee na kazi