• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
MATHEKA: Zogo kuhusu sare za polisi ni hatari kwa usalama wa nchi

MATHEKA: Zogo kuhusu sare za polisi ni hatari kwa usalama wa nchi

Na BENSON MATHEKA

RIPOTI kuhusu mafundi mitaani wanaoshona sare za polisi na kuzuizia maafisa hao wa usalama ni za kutisha.

Hii ni kwa sababu wahalifu wanaweza kununua sare hizo na kuzitumia kuhangaisha umma wakijifanya polisi halali.

Hatua hii inaonyesha kuwa, serikali haikuweka mikakati ya kutosha ilipobadilisha sare za polisi miaka miwili iliyopita.

Kwa kuwasukuma polisi kuvalia sare hizo kabla ya kuhakikisha kila afisa amezipata, wakuu wa polisi walifungulia milango maafisa hao kuzipata kwa mafundi wa mitaani.

Kwa kufanya hivyo, pia waliwafungulia wahalifu fursa ya kununua sare hizo na kuzitumia kuhangaisha umma.

Ilipotangaza uamuzi wa kubadilisha sare hizo, Wizara ya Usalama wa Ndani ilisema kwamba, ilichagua rangi ya nguo ambayo sio rahisi kupatikana mitaani.

Ilisema kwamba, sare hizo zingeshonwa kwa awamu na kitengo cha kutengeneza sare za maafisa wa usalama na shirika la vijana wa Huduma ya Taifa (NYS).

Inashangaza basi, sare hizo zinaweza kushonwa na mafundi wa mitaani miaka miwili baadaye.

Swali linalowatia hofu raia ni je, ni wahalifu wangapi ambao tayari wamenunua sare hizo? Je, wataweza kuamini kwamba kila anayevalia sare hizo ni afisa wa polisi? Sio mara ya kwanza Wakenya kuhangaishwa na wahalifu wanaovalia sare za polisi. Sio mara moja wahalifu wamekamatwa wakiwa na magwanda rasmi ya polisi na kushtakiwa mahakamani kwa kupatikana na mali ya serikali.

Ikizingatiwa kwamba ni maafisa wa polisi wanaonunua sare hizi kutoka kwa mafundi wa mitaani na ni wao wanaofaa kuwakamata wanaohusika na biashara hiyo, itakuwa vigumu kwa wanaozishona kuchukuliwa hatua za kisheria.

Pili, kuwakamata itakuwa ni kuwahangaisha kwa kufanya kazi yao. Tatu, itakuwa vigumu kwa mafundi hao kutofautisha afisa wa polisi na wahalifu ambao wanaweza kutumia fursa hii kununua sare hizi.

Badala ya kukanusha kwamba maafisa wa polisi wananunua sare hizi mitaani kwa sababu wanalazimishwa kuzivaa na wakubwa wao, wakuu wa polisi wanavaa kueleza umma mafundi hawa wanapopata vitambaa za rangi ambayo serikali ilisema ilichagua kwa sababu sio rahisi kupatikana.

Ujasiri ambao mafundi hao wako nao unaonyesha kuna watu wenye ushawishi wanaowalinda. Ukweli ni kuwe na njama au la, upatikanaji wa sare za polisi kiholela ni hatari kwa usalama wa nchi.

You can share this post!

ODONGO: Matamshi ya Raila Jr si uasi dhidi ya baba yake

Caleb achaguliwa mwenyekiti FKF Nairobi Magharibi, Maureen...