ONGAJI: Nani ataokoa maisha ya vijana?
Na PAULINE ONGAJI
Kila unapotembea katika mitaa na miji mingi hapa nchini Kenya, huenda umekutana na vikundi vya vijana –wa kike na kiume – wakiwa wamevalia magwanda ya kazi za sulubu, huku wakiwa na ala za shughuli hii kama vile vifagio, sepetu na kifyekeo miongoni mwa zingine.
Hapa, wanakumbwa na kibarua kigumu cha kufanya kazi za sulubu kama vile kukata nyasi, kuokota taka na kuzibua mitaro na mabomba ya majitaka, vyote chini ya mradi wa ‘kazi mtaani’.
Kupitia mradi huu naelewa kwamba wanapaswa kujipatia mapeni kidogo, huku nao wakitarajiwa kutoa huduma zao ili kunufaisha jamii.
Na sipo hapa kukosoa mradi huu, lakini bila shaka picha hii ya kuhuzunisha inathibitisha hali ngumu ya kiuchumi ambayo inaendelea kuwakumba vijana wetu.
Pengine utajiuliza kwa nini nasema hivi? Huku mataifa mengine ulimwenguni yakiwekeza mabilioni ya pesa kwa miradi ya kielimu, kiteknolovia na uvumbuzi ili kuwasaidia vijana, hii leo katika karne ya 21, sisi hapa tunawapa vijana wetu ala hizi kama mbinu ya kuwapa fedha kidogo.
Kuna baadhi ya watu wanaoohoji kwamba hii inasaidia kwa kuhakikisha kwamba vijana hawa wanapata hela mifukoni, lakini tena swali ni pesa ngapi hizo wanazolipwa kwa shughuli hii ya mchana kutwa?
Mradi huu unapaswa kuendelea kwa muda upi? Je pesa hizi zinatosha kuwasaidia kununua chakula chao cha kila siku, au hata kuanzisha mradi wa kujisaidia baadaye maishani?
Hii inanikumbusha kisa cha majuma machache yaliyopita ambapo nikiwa kwenye kiuo cha mabasi, niligundua kwamba kuna vijana ambao kwa shilingi kumi au 20, wako tayari kukuhifadhia kiti kwenye gari, hasa wakati wa jioni ambapo watu wengi wanarejea nyumbani.
Au kikundi cha wasichana niliokutana nao wakitembea mtaani katika harakati za kuuza sabuni.
Hii tu ni baadhi ya mifano ya masaibu ambayo yamekuwa maisha ya kawaida kwa vijana wengi humu nchini. Haya yanajiri huku kila siku vyombo vya habari vikiendelea kuangazia hadithi za vijana ambao licha ya kuelimika, wamesalia kufanya vibarua vya sulubu.
Kuna baadhi ya watu wanaohoji kwamba utakuwa upumbavu kutegemea tu masomo, badala ya ujuzi ambao waweza kukuletea riziki. Na mara ingine nakubaliana na wazo hili, lakini ikiwa hii ndio hatima ya asilimia kubwa ya vijana wanaohitimu kila mwaka, basi kuna tatizo kubwa sio tu kwa mfumo wetu wa elimu, bali jamii yetu kwa ujumla.
Lakini pia kwa upande mwingine, cha muhimu sio tu kuwa na hati za vyuoni, bali ujuzi wa kuweza kufanya kazi uliyosomea, na swali ni wangapi wanaohitimu kila mwaka wana uwezo wa kufanya walichosomea.
Kwa mfano, kila mwaka maelfu ya wanafunzi waliosomea uhandisi vyuoni uhitimu, ila ni wangapi tunaowaona wakitumia ujuzi wao kila kunapokuwa na miradi mikubwa ya uhandisi nchini. Sio suala la kupewa fursa, lakini swali ni je ni wangapi wanaoweza fanya kazi hii?
Nikirejelea suala la hatima ya vijana, ni wakati wa viongozi kuelewa kwamba kukosa kuwekeza katika vijana kutachochea masaibu ya kijamii, kisiasa na kiuchumi katika siku zijazo. Hii inamaanisha kwamba, jinsi mambo yalivyo, hali ilivyo sasa ni hatari sio tu kwa vijana, bali kwa jamii yote ya Kenya kwa ujumla.