• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:46 PM
Johana aisaidia timu yake kupiga hasidi 4-1

Johana aisaidia timu yake kupiga hasidi 4-1

Na GEOFFREY ANENE

Eric Johana Omondi alifunga tobwe la kombora katika Ligi ya Daraja ya Pili Uswidi akisaidia Jonkopings Sodra kupepeta Osters 4-1, Jumamosi.

Kiungo huyo mshambuliaji mwenye umri wa miaka 26, ambaye alianzishwa kwenye kiti, alipachika bao hilo sekunde chache baada ya kujaza nafasi ya Kevin Rodeblad Lowe dakika ya 46.

Bao hilo lake la saba ligini msimu huu lilipatikana baada ya kumegewa pasi kutoka kwa beki Jesper Svensson pembeni kushoto na kuchenga mabeki watatu na kusukuma shuti kali kutoka nje ya kisanduku hadi wavuni.

Lilifungulia Jonkopings milango ya mabao zaidi kutoka kwa mshambuliaji Edin Hamidovic dakika ya 73 na 85 na beki Jetmir Haliti dakika ya mwisho ya majeruhi. Omondi pia alionyeshwa kadi ya njano dakika ya 53.

Osters ilikuwa ya kwanza kuona lango kupitia kwa kiungo Carl Johansson dakika ya 41. Jonkopings ni ya tatu kwenye ligi hiyo ya timu 16 kwa alama 35 kutokana na mechi 19. Degerfors na Halmstad zinashikilia nafasi mbili za kwanza kwa alama 40 na 37 baada ya kusakata mechi 18 kila moja.

Kwenye Ligi Kuu ya Uswidi, AIK itavaana na Hammarby leo Jumapili. Beki wa kupanda na kushuka wa AIK, Eric “Marcelo” Ouma Otieno hajajumuishwa katika kikosi cha Bartosz Grzelak kitakachosakata mchuano huo kumaanisha kuwa bado hajafikia kiwango cha kupatiwa dakika uwanjani.

Marcelo amekuwa akifanya mazoezi tangu Juni katikati. Aliumia mguu wake wa kushoto mazoezini Mei 29 na kufanyiwa upasuaji Mei 30.

Alitarajiwa kuwa nje kwa kati ya wiki sita na nane, lakini wiki 16 sasa zimepita. Hata hivyo, amekuwa akichapisha video kwenye mitandao yake ya kijamii kupasha mashabiki habari anavyoendelea. Mnamo Septemba 6, Marcelo alisema ni muda tu kabla arejee uwanjani.

Timu yake ya AIK, ambayo inashikilia nafasi ya 13, moja nje ya mduara hatari wa kutemwa, imekuwa ikifanya vibaya. Ilishinda mechi yake ya kwanza katika mechi nane ilipozaba Helsingborg 2-0 Agosti 23. Imeambulia alama moja katika mechi mbili zilizopita baada ya kutoka 0-0 dhidi ya viongozi Malmo hapo Septemba 13.

Nayo Elfsborg ilikaribisha beki Joseph Stanley Okumu kutoka marufuku ya mechi moja ya kadi za njano ikitoka 2-2 dhidi ya Mjallby hapo Septemba 17. Elfsborg, ambayo inakamata nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu Uswidi, itarejea uwanjani hapo Septemba 21 kumenyana na nambari mbili Hacken.

  • Tags

You can share this post!

Timu ya Origi yakabwa ligini

Mechi mbili za kwanza za Leeds United katika EPL zazalisha...