Michezo

Mechi mbili za kwanza za Leeds United katika EPL zazalisha mabao 14!

September 21st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

LEEDS United waliwapokeza Fulham kichapo cha 4-3 kwenye mchuano wao wa kwanza wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) katika uwanja wa nyumbani baada ya miaka 16.

Mechi mbili za kwanza za Leeds katika EPL muhula huu zimeshuhudia jumla ya mabao 14 yakifumwa wavuni, hii ikiwa idadi ya juu zaidi kuwahi kushuhudia tangu 1962-63. Msimu huo, Wolves walifunga mabao 12 nao wakaokota wavuni magoli mawili katika gozi la EPL.

Baada ya kupokezwa kichapo cha 4-3 kutoka kwa Liverpool uwanjani Anfield mnamo Septemba 12, Leeds ya kocha Marcelo Bielsa ilijinyanyua dhidi ya Fulham ambao ni limbukeni wenzao kwenye kampeni za msimu huu ligini.

Helder Costa aliwaweka wenyeji Leeds kifua mbele katika dakika ya tano kabla ya Aleksandar Mitrovic kusawazisha kupitia penalti ya dakika 34 iliyochangiwa na Robin Koch aliyemchezea visivyo kiungo Joe Bryan.

Leeds walirejea uongozini katika dakika ya 41 baada ya Mateusz Klich ambaye ni raia wa Poland kufunga penalti iliyosababishwa na Bryan aliyekabili kivoloya fowadi Patrick Bamford.

Bamford aliwafungia Leeds bao la tatu kunako dakika ya 50 kabla ya Costa kupachika wavuni goli la nne dakika saba baadaye.

Ingawa hivyo, Bobby Decordova-Reid na Mitrovic waliwarejesha Fulham mchezoni mwishoni mwa kipindi cha pili kwa kufunga mabao mawili ya haraka katika dakika za 62 na 67 mtawalia.

Wakicheza dhidi ya Leeds mnamo Septemba 12, Liverpool ambao walitawazwa mabingwa wa EPL kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30 msimu uliopita, walioongoza mechi mara tatu huku Leeds wakitoka nyuma kila mara na kusawazisha.

Ilikuwa penalti ya dakika ya mwisho kutoka kwa fowadi Mohamed Salah ndiyo iliyowezesha Liverpool kuwazamisha Leeds kwa mabao 4-3 katika mechi hiyo ya ufunguzi wa msimu mpya wa 2020-21.

Penalti iliyofumwa wavuni na Salah ilitokana na tukio la sajili mpya wa Leeds, Rodrigo Moreno, kumchezea Fabinho visivyo katika dakika ya 88.

Salah aliyefunga mabao matatu katika mechi hiyo, alifungua ukurasa wa magoli kunako dakika ya nne kupitia penalti baada ya beki raia wa Ujerumani, Robin Koch kunawa mpira.

Hata hivyo, Leeds walisawazisha kupitia kwa Jack Harrison katika dakika ya 12 kabla ya masihara ya mabeki yao kumruhusu difenda Virgil van Dijk kurejesha Liverpool uongozini katika dakika ya 20.

Mechi hiyo ilishuhudia refa akikataa kuhesabu jumla ya mabao manne. Dalili zote ziliashiria kwamba Leeds wangaliondoka Anfield wakiwa na alama moja kapuni baada ya Mateusz Klich kufunga bao la kusawazisha katika dakika ya 66.

Liverpool waliendeleza rekodi yao ya kutoshindwa katika uwanja wao wa nyumbani katika jumla ya mechi 60 za EPL. Kufikia sasa, miamba hao wameibuka na ushindi katika mechi 49 na kuambulia sare mara 11.

Chelsea waliwahi kupiga jumla ya mechi 86 bila ya kushindwa katika uwanja wao wa Stamford Bridge kabla ya rekodi hiyo kukomeshwa mnamo Oktoba 2008. Awali, Liverpool walikuwa wamepiga jumla ya mechi 63 bila ya kushindwa hadi kufikia Disemba 1980.

Ilikuwa mara ya pili kwa mechi ya kwanza ya msimu mpya wa EPL kushuhudia jumla ya mabao matano yakifungwa kufikia mwisho wa kipindi cha kwanza. Manchester United waliwahi kupiga Fulham 5-1 mnamo Agosti 2006 huku Man-United wakiongoza kwa 4-1 kufikia mwisho wa kipindi cha kwanza.

Ilikuwa pia mara ya kwanza kwa Liverpool kufungwa mabao matatu katika mechi ya ligi nyumbani tangu Septemba 1982.

Liverpool kwa sasa wameshinda kila mojawapo ya mechi zao 35 zilizopita ligini ambapo Salah amefunga. Raia huyo wa Misri amevunja rekodi ya Wayne Rooney aliyewahi kufunga jumla ya mabao 34 mfululizo katika mechi zilizoshuhudia Man-United wakiibuka washindi kati ya Septemba 2008 na Februari 2011.

Liverpool walikuwa wenyeji wa Chelsea ligini mnamo Septemba 20, 2020 uwanjani Stamford Bridge.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO