Mbappe arejelea kipute cha Ligue 1 kwa mbwembwe
Na MASHIRIKA
CHIPUKIZI Kylian Mbappe alirejea kuchezea Paris Saint-Germain (PSG) kwa vishindo mnamo Septemba 20, 2020 alipofunga bao na kusaidia waajiri wake kuwapepeta Nice 3-0 katika Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1).
Mbappe alikuwa amekosa mechi zote tatu za ufunguzi wa msimu huu baada ya kuugua Covid-19 kwa mara ya pili. Katika kipindi hicho, PSG walipoteza mechi mbili na kushinda mchuano mmoja.
Fowadi huyo raia wa Ufaransa aliwafungulia PSG ukurasa wa mabao kupitia penalti ya dakika ya 38 baada ya kuchezewa visivyo na Kephrem Thuram ndani ya kijisanduku.
Angel Di Maria alifunga bao la pili kutokana na fataki ya Mbappe iliyopanguliwa na kipa wa Nice mwishoni mwa kipindi cha kwanza kabla ya Marquinhos kufunga la tatu katika dakika ya 66.
Goli lilijazwa kimiani na Mbappe kunako dakika ya 75 halikuhesabiwa na refa kwa sababu fowadi huyo wa zamani wa AS Monaco alikuwa ameotea.
PSG walikosa huduma za Layvin Kurzawa, Leandro Paredes na mshambuliaji Neymar Jr katika gozi hilo. Watatu hao walipigwa marufuku wikendi iliyopita kwa kuzua vurugu mwishoni mwa mechi ya Ligue 1 iliyowakutanisha na Olympique Marseille walioibuka washindi kwa 1-0 katika mechi hiyo ugani Parc des Princes.
Chini ya kocha Patrick Vieira ambaye ni mwanasoka wa zamani wa Arsenal, Nice sawa na mabingwa watetezi PSG, kwa sasa wanajivunia alama sita kutokana na mechi nne zilizopita za Ligue 1.
TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO