Habari

Magoha azidi kukoroga elimu

September 22nd, 2020 Kusoma ni dakika: 3

VALENTINE OBARA na JOSEPH OPENDA

WAZIRI wa Elimu, Prof George Magoha, Jumatatu aliendelea kuwakoroga akili wazazi, walimu na wanafunzi kuhusu hatima ya masomo aliposhindwa tena kutoa mwelekeo thabiti.

Waziri pia alionyesha upuuzaji mkubwa wa masuala muhimu na ya msingi kuhusu elimu.

Hapo jana alikariri kuwa uamuzi wa mwisho kuhusu tarehe ya kufungua shule haujafanywa, lakini wakati huo huo akasema wakati umefika watoto kurudi shuleni.

Pia aliagiza walimu wote kuanza kurudi shuleni kwa maandalizi ya ufunguzi, na kuwaacha bila kujua watafanya maandalizi hayo kwa muda gani.

Kuchanganyikiwa huku kwa Wizara ya Elimu kumzua kizaazaa, wazazi wengi wakisema hawako tayari kupeleka watoto wao shuleni hadi Januari mwaka ujao kama ambavyo Prof Magoha alivyokuwa amewahakikishia mnamo Julai.

Wakati huo Prof Magoha alisema mwaka wa masomo wa 2020 umefutiliwa mbali na wanafunzi watarudia madarasa walimokuwa 2021. Pia alifutiliwa mbali mitihani ya kitaifa.

Lakini uamuzi wa kufungua shule kabla ya 2021 umewakanganya wazazi ambao wanasema hali ya uchumi imevurugwa mno na janga la corona, kwa hivyo hawana uwezo wa kugharamia elimu kwa sasa.

Akijibu kilio cha wazazi, Waziri Magoha jana aliwapuuzilia mbali akidai kuwa elimu ni ya bure katika shule za umma.

“Ukimpeleka mtoto katika shule ya kibinafsi itabidi ulipe. Usipoweza kulipa mlete mtoto wako katika shule ya umma na tutamchukua. Kwa shule za upili, karibu asilimia 75 ya shule zetu ni za kutwa na hazihitaji malipo,” akasema.

Kwa upande mwingine, waziri alisema masomo katika shule za upili za bweni hugharamiwa na serikali huku wazazi wakilipia tu chakula, ambacho kulingana na Prof Magoha mtoto angekula hata akiwa nyumbani.

Hii ni licha ya Prof Magoha kujua kuwa hata katika shule za umma hasa sekondari karo ni ya juu.

Pia alionekana kupuuza ukweli wa mambo kuwa shule haziwezi kuendeshwa bila pesa kwa kutaka walimu wavumilie wasio na karo: “Walimu si Wanyama, kama kuna tatizo wataelewa,” akaeleza.

Kwa kuambia wazazi walio na wanafunzi katika shule za kibinafsi wawapeleke za umma, Waziri alionekana kusahau kuwa tayari zina ubaba wa madarasa na kuna misongamano ambayo huchangia maambukizi ya corona.

Kuanzia shule za msingi hadi upili, nyingi hutatizika kupata miundomsingi na rasilimali za kutosheleza mahitaji ya kila mwanafunzi.

Endapo wazazi wote waliolemewa kiuchumi wataamua kuhamisha watoto wao hadi shule za umma kutoka kwa za kibinafsi, hii itasababisha balaa shuleni.

Prof Magoha pia alionyesha kufungia macho ukweli kuwa Baraza la Mitihani ya Kitaifa (KNEC) lilikuwa tayari limekamilisha usajili wa watahiniwa. Hivyo basi haijulikani hatua itakayochukuliwa kwa watahiniwa ambao watahitaji kuhamishwa hadi shule za umma kutoka kwa walikojisajili.

Katika juhudi za kujaribu kuboresha hali shuleni kabla watoto warudi, serikali iliamua kutumia Sh1.9 bilioni kuunda madawati na viti ambavyo vitapelekwa kwa shule za msingi na upili.

Lakini baadhi ya wadau wameibua swala kuhusu uhaba wa madarasa ambayo watoto watatumia na hayo madawati.

Jumatatu, Prof Magoha alisisitiza watoto wanahitaji madawati na mpango huo hautasitishwa.

“Huwa nashangaa wakati wengine wanauliza kama watoto wanahitaji madawati. Tayari tulikubaliana kuwa masomo yanaweza kufanyika uwanjani,” akaeleza.

Mpango huu wa kuweka madarasa nje haujazingatia masuala kama vile mvua, jua kali, upepo miongoni mwa hali nyingine za hewa pamoja na usalama wa wanafunzi.

Pendekezo la kufungua shule kabla ya Januari 2021 lilitolewa kwa msingi wa jinsi idadi ya maambukizi ya virusi vya corona inavyoendelea kuwa ya chini kwa takriban wiki tatu sasa. Hii inaambatana na kupungua kwa upimaji.

Licha ya idadi kupungua, kuna wazazi ambao bado wana hofu kuhusu usalama wa watoto wao watakapokuwa shuleni.

Hii ni kutokana na kuwa, kando na utengenezaji madawati na barakoa zinazonuiwa kusambaziwa wanafunzi, serikali haijafafanua zaidi kuhusu mipango itakayotumiwa kuhakikisha wanafunzi, walimu na wafanyakazi wengine wote shuleni wanatimiza kikamilifu kanuni za kuepusha maambukizi ya virusi vya corona.

Kwingineko, mzazi alielekea mahakamani kupinga hatua ya serikali kufutilia mbali kalenda ya shule mwaka 2020.

Dkt Benjamin Magare Gikenyi aliwasilisha ombi katika Mahakama Kuu ya Nakuru akitaka uamuzi uliotangazwa na Prof Magoha ubatilishwe.