• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 11:05 AM
DENNIS MUDI: Machozi ya furaha kijana kupata fursa adimu ya kumhoji Rais Kenyatta

DENNIS MUDI: Machozi ya furaha kijana kupata fursa adimu ya kumhoji Rais Kenyatta

Na DIANA MUTHEU

KWA siku nne sasa, Dennis Mudi amekuwa gumzo katika mitandao tofauti ya kijamii.

Video moja iliyosambaa katika majukwaa ya mitandao kama Facebook, Twitter, na YouTube, pamoja na majukwaa ya habari imevutia hisia mseto. Inamwonyesha Dennis alionekana kujawa na hisia kiasi kwamba anaangua kilio cha furaha alipopewa ruhusa ghafla ya kumhoji Rais Uhuru Kenyatta akiwa katika bustani ya Mama Ngina Waterfront, Mombasa.

Rais Kenyatta alikuwa amezuru bustani hilo akiwa katika ziara yake ya Pwani kuangalia miradi mbalimbali inayoendelea.

Katika mahojiano na Taifa Leo mnamo Jumatatu akiwa eneo la Shanzu, Dennis alisimulia kuwa alikuwa katika likizo na aliamua kufika katika bustani hiyo akiwa pamoja na wenzake baada ya kusikia sifa zake, na hapo ndipo alikutana na Rais Kenyatta.

“Sikutarajia kuwa Rais Kenyatta angetembelea eneo hilo. Alinikuta nikiwa katika shughuli zangu za kuwahoji wafanyabiashara waliokuwa wakiuza koa (shells) na kufurahishwa na kazi yetu, ndipo akanipa ruhusa nimhoji,” akasema Dennis.

Kijana huyu ni mkazi wa Lurambi katika Kaunti ya Kakamega na ni mtoto wa tatu katika familia ya watoto wanne.

Dennis ni mtangazaji anayeinukia katika jukwaa la mtandaoni MKTV lililoanzishwa mwaka 2017, na huwa anafanya kipindi kimoja kiitwacho ‘Hustle Mtaani’ ambapo huwa anawaangazia watu wenye biashara ndogondogo katika sehemu tofauti za nchi.

“Nilijawa na furaha hadi nikaanza kulia machozi ya furaha lakini ovyo kabisa kwa kuwa si rahisi kwa mtu yeyote hata wanahabari waliobobea kumhoji Rais. Sikumuuliza chochote ila tu nilibakia kumshukuru, na alipoona kuwa nimeshindwa kuzungumza, aliamua kueleza wananchi baadhi ya mambo ambayo alikuwa anatekeleza katika ziara yake ya Mombasa,” akasema.

Mtangazaji huyo anasema jukwaa hilo lao linaendeshwa na vijana 14 ambao wamejitolea bila malipo.

Anasema miongoni mwao ni msichana mwenye ugonjwa wa mtindio wa ubongo (celebral palsy).

“Maono yetu ni kuwa runinga nambari moja nchini inayowasaidia wafanyabiashara wadogowadogo nchini kujikuza kwa kuwaangazia na kuwafanya wafahamike kote nchini,” akasema Dennis.

Aidha anasema kuwa kiuongozi wa nchi alimuahidi kuwa siku moja atamwalika katika Ikulu ili aweze kumhoji kisawasawa.

“Baada ya dakika 30 nilipokea simu kutoka kwa Ikulu ya Mombasa na nikaelezwa kuwa saa moja asubuhi siku ifuatayo nifike pale kumwona Rais. Niliamka mapema, na nilipofika pale nilielezwa kuwa nitapangiwa siku maalum ya kukutana na Rais katika Ikulu ya Nairobi,” akasema kijana huyo.

Kupitia runinga ya mtandaoni ya Dennis na wenzake, Rais Kenyatta alisema kuwa atafungua Mama Ngina Waterfront ili wananchi waweze kuzuru eneo hilo na kujivinjari.

“Tutafungua ndipo wafanyabiashara hao pia waweze kurejea katika shughuli zao za kawaida na pia wapate wateja wengi zaidi,” akasema Rais Kenyatta.

Pongezi

Pia, alipongeza Dennis na mwenzake kwa kutia bidii na kujitahidi kufanya kazi zao.

“Nimewaona mkiendeleza kazi zenu na ni hatua nzuri. Lazima vijana kama nyinyi kujitahidi ili kumudu mahitaji muhimu,” alisema Rais Kenyatta.

Baadhi ya watu wakitumia majukwaa ya mtandaoni walimsuta kwa kulia ovyo, huku wengine wakimpa moyo kupitia jumbe zao wakisema, hata wao wangepata hisia kama hizo iwapo wangepata nafasi ya kumhoji Rais.

Mtangazaji maarufu wa Kiss 100, Felix Odiwuor maarufu Jalang’o aliweka kijisehemu cha video hiyo katika mtandao wake wa Instagram huku akiwauliza watu wanaomfuatilia watoe maoni yao kuhusu jinsi Dennis alivyotumia fursa hiyo.

Baadhi ya watu maarufu walichangia mada hiyo na msanii tajika, Khaligraph Jones alisema katika ujumbe: “Jamaa yuko sawa. Natumai chaneli yake katika mtandao wa YouTube itapata wafuasi wengi; hisia kama hizo hutokea.”

Naye, chale – mcheshi – Oliver Otieno maarufu YY aliwasuta watu waliozungumza mabaya kumhusu Dennis na kuwaambia kuwa hisia kama hizo huweza kumtokea mtu yeyote akiwa karibu na mtu mashuhuri kama Rais Kenyatta.

“Watu wanaongea na hata wakipewa ruhusa kuzungumza na msichana wanaanza kutazama ukuta ama jua linavyowaka,” akasema YY katika ujumbe.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Usawa wahitaji suluhu la kudumu

PSC kupambana na Maraga kortini