KAMAU: Viongozi wapalilie historia kwa kuandika vitabu vyao
Na WANDERI KAMAU
UANDISHI wa vitabu ndio mbinu bora zaidi ya mwanadamu kunakili na kuhifadhi kumbukumbu ya muhimu duniani tangu jadi.
Kabla ya ujio wa karatasi mwanzoni mwa karne ya 15, jamii za kale zilikuwa zikiandika masuala muhimu kwenye mawe au madaftari maalum yaliyotengenezwa kwa majani na maganda ya miti.
Bila shaka, hilo lilikuwa dhihirisho tosha kwamba maisha ya mwanadamu kamwe hayawezi kuwa kamilifu bila uhifadhi wa kumbukumbu muhimu zinazohusu mabadiliko yake.
Utambuzi huo ndio ulikuza mfumo wa elimu katika baadhi ya nchi kama Ugiriki, ambayo inatajwa kuwa kitovu cha elimu ya kisasa duniani.
Kadri nyakati zilivyosonga, jamii nyingi ziliendelea kukumbatia elimu na uandishi wa vitabu kama mojawapo ya njia muhimu za kuleta ustawi katika nyanja za kisiasa na kiuchumi.
Mafanikio zaidi yalipatikana kwenye jamii ambazo zilipitisha mtindo huo kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
Kimsingi, miongoni mwa nchi ambazo zilikumbatia mwelekeo huo ni Amerika, ambapo tangu 1776 ilipojinyakulia uhuru wake kutoka kwa Uingereza, imekuwa kawaida kwa kila rais anayemaliza kipindi chake kuandika kitabu kuelezea aliyokumbana nayo.
Ni hali ambayo imedhihirika miongoni mwa marais wa awali kama Thomas Jefferson, Theodore Rooselvet, Bill Clinton, George Bush na sasa Barack Obama.
Wiki iliyopita, Bw Obama alitangaza kuwa yuko katika hatua za mwisho kumalizia kitabu ‘A Promised Land’ (Nchi ya Ahadi) kinachorejelea safari yake kama rais wa Amerika kati ya 2008 na 2016.
Kitabu hicho kinatarajiwa kuzinduliwa rasmi baada ya taifa hilo kushiriki kwenye uchaguzi wa urais mnamo Novemba.
Kimsingi, tangazo la Bw Obama limedhihirisha kuwa ni mtindo wa marais wa Amerika kuandika vitabu kurejelea matukio yote muhimu yaliyokumba tawala zao.
Ingawa kuna hisia miongoni mwa wakosoaji wake kuwa hakutimiza baadhi ya ahadi alizotoa, la muhimu ni kwamba, kwa kuchapisha kitabu hicho, atapata nafasi mwafaka kujieleza mwenyewe.
Licha ya utawala wake kukosolewa pakubwa, Rais Donald Trump pia amechukua mkondo huo huo, kwani kuna vitabu kadhaa ambavyo tayari vimeandikwa kuhusiana na serikali yake.
Kile kinajitokeza hapa ni kuwa, kwa mwelekeo huo, imekuwa kama jukumu marais hao kuielezea jamii kwa kina kuhusu sababu za kuchukua ama kutochukua hatua fulani wakiwa uongozini.
Kinaya ni kuwa, hali hiyo ni kinyume na ilivyo nchini Kenya na bara Afrika kwa jumla.
Ingawa kuna vitabu kadhaa ambavyo vimeandikwa kuwahusu marais wa awali kama Mzee Jomo Kenyatta, Daniel Moi na Mwai Kibaki, hakuna hata kimoja kinachojumuisha maelezo yao moja kwa moja.
Badala yake, vingi vinahusisha kauli na hisia za washirika wao wa karibu, hali inayowanyima Wakenya na vizazi vijavyo nafasi ya kufahamu kwa undani historia ya nchi.
Kama Amerika na mataifa mengine ya Magharibi, wakati ni sasa kwa wanasiasa nchini kukumbatia uandishi wa vitabu kuikuza nchi, demokrasia na kwa manufaa ya vizazi vijavyo. Hawamfaidi yeyote wanapofariki na siri za baadhi ya matukio muhimu yaliyoikumba nchi enzi zao.