• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 6:27 PM
WAKFU WA AGA KHAN: Uchambuzi wa hadithi ‘Maguru Apatiana Miguu’

WAKFU WA AGA KHAN: Uchambuzi wa hadithi ‘Maguru Apatiana Miguu’

Na WANDERI KAMAU

Mwandishi: Mutugi Kamundi

Mchapishaji: African Storybooks Initiative

Mhakiki: Wanderi Kamau

Kitabu: Novela ya Watoto

Mtafsiri: Ursula Wafula

Jina la Utungo: Maguru Apatiana Miguu

HAMJAMBO watoto? Je, mshawahi kufikiri kwanini jongoo ana miguu mingi na nyoka hana hata mmoja?

Je, mbona wanyama wengine wana miguu minne na wengine miwili pekee?

Hapo zamani wanyama wote hawakuwa na miguu isipokuwa binadamu. Wote walikuwa wakitambaa kama nyoka.

Hata hivyo, mtawala mkuu wa wanyama hao, ambaye aliitwa Maguru, aliamua kuwapa wanyama miguu.

Lengo kuu lilikuwa kuwaondolea uchungu waliopata wakitambaa bila miguu – tumbo zao zilikwaruzwa.

Tangazo la Maguru liliwafurahisha sana wanyama wengi, na walianza kusherehekea hata kabla siku yenyewe kufika. Waliimba na kucheza.

Kwa kupata miguu wangeweza kusimama, kutembea na kuona mbali.

Siku ilipofika, wote waliandamana kwenda kwa Maguru ili kupewa miguu.

Kila mnyama alipata miguu minne huku kila ndege akipewa miguu miwili.

Sura zao zilibadilika sana waliposimama baada ya kupewa miguu.

Baadhi yao hata walianguka waliposimama.

Wakiwa wenye furaha kubwa, walizunguka kote kijijini wakiwaambia watu: “Hatutatambaa tena.”

Lakini sio wanyama wote walifanikiwa kufika kwa Maguru wakati ule; jongoo na nyoka walibaki nyuma.

Jongoo alipowasili kwa Maguru na kuulizwa ikiwa kuna mnyama mwingine aliyesalia, alimjibu kwa kusema: “La. Mimi ndiye wa mwisho.”

Maguru alipotazama hifadhi yakee aligundua kuna miguu mingi sana iliyokuwa imebaki.

Alishangaa aifanyie nini ilhali ni jongoo pekee aliyekuwa amebaki.

Baada ya kufikiri kwa muda alijiambia: “Ikiwa yeye ndiye wa mwisho, nitaifanyia nini miguu iliyobaki?”

Akaamua kumpa jongoo miguu hiyo yote.

Jongoo aliondoka kwa Maguru akiwa amejawa na furaha.

Moyoni alihisi kwamba sasa angeweza kwenda kwa kasi zaidi kuwaliko wanyama wote waliomtangulia, kwani ndiye alikuwa mwenye miguu mingi zaidi.

Baada ya jongoo kuondoka, nyoka alifika kwa Maguru akimsihi ampe miguu kama wanyama wale wengine.

“Tafadhali nipatie nami miguu,” akasihi.

Hata hivyo, Maguru alimwambia hakukuwa na miguu yoyote iliyobaki kwani alishapeana yote.

“Wewe ulikuwa wapi?” akauliza Maguru akimtaka nyoka kueleza alikokuwa wakati wanyama wengine walikuwa wakipewa miguu.

Cha kushangaza, nyoka alisema alilala kupita kiasi ndipo akachelewa.

Maguru alitafuta miguu kote kote lakini akakosa. Nyoka hakufanikiwa kupata miguu.

Hiyo ndiyo sababu nyoka hawalali; daima huwa wanasubiri kupata miguu.

Funzo kuu kwenye hadithi hii ni kwamba, umoja una manufaa sana katika jamii.

Kwa mfano, ni kwa umoja ambao wanyama wengine walionesha ndiposa wakaandamana wote kuelekea kwa Maguru kupewa miguu.

Pia tunajifunza kwamba tusiwe wenye ubinafsi kama jongoo.

Jongoo angeuliza wenzake iwapo kulikuwa na mnyama mwingine aliyebaki nyuma, kabla kuchukua miguu yote.

Vile vile, yeye ni mnyama aliyejipenda. Kujipenda kwake kunaonekana pale anaposema atakuwa akienda kwa mwendo wa kasi zaidi kuliko wanyama wote.

Mwisho, tunafunzwa kuwa uvivu si mzuri. Kwa mfano, uvivu wa nyoka kushindwa kuamka mapema ndiyo sababu ilimfanya asipate miguu.

Ni hadithi inayoeleweka virahisi kwani kuna picha kem kem za wanyama.

Soma hadithi hii au itazame katika runinga yako ya NTV kila Jumatatu kuanzia saa moja na dakika 50 usiku.

[email protected]

You can share this post!

Kinara wa upinzani aikosoa serikali kwa kumhangaisha

MWALIMU KIELELEZO: Millicent Loice Achieng