• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
DPP aahidi kunasa wafisadi wa vyeo vya juu serikalini

DPP aahidi kunasa wafisadi wa vyeo vya juu serikalini

Na BENSON MATHEKA

Mkurugenzi mpya wa Mashtaka ya Umma (DPP) Bw Noordin Haji ameahidi kuleta mwamko mpya katika vita dhidi ya ufisadi kwa kukabili wezi wa mali ya umma bila kujali vyeo vya wanaohusika.

Kwenye mahojiano, Bw Haji amesema atafufua vita dhidi ya ufisadi akitaja kufungwa jela kwa waliokuwa maafisa wakuu wa jiji la Nairobi wiki jana kama onyo kwamba maafisa wakuu wa serikali wanaokabiliwa na kesi za ufisadi.

“Ninaelewa kwamba Wakenya wamevunjika moyo. Hata mimi nimechoka. Kulikuwa na kuna kesi dhidi ya wanaoitwa watu wakubwa.

Kuna baadhi yao ambao wamefungwa jela, hivi punde ikiwa ni aliyekuwa katibu wa kudumu Sammy Kirui na wengine.

Kuna kesi dhidi ya mawaziri, makatibu wa wizara, wakuu wa mashirika ya serikali, wabunge, magavana na maafisa wakuu wa serikali za kaunti. Nitazidisha juhudi za kupiga vita ufisadi na uhalifu wa uchumi,” alionya Bw Haji.

Wadidisi wanasema Bw Haji akihakikisha uchunguzi wa kesi utafanywa vyema, washtakiwa watapatikana na hatia.

“Tatizo la ufisadi ni kuwa uchunguzi huwa duni na hii hufanya kesi nyingi kutupiliwa mbali kisha mahakama zinalaumiwa. Uchunguzi ukifanywa vyema na kwa kina, watu watafungwa jela kwa kutumia mamlaka yao vibaya kula mlungula,” asema Wakili Jane Wangari.

Hata hivyo, anahisi kwamba kesi za ufisadi zimekuwa zikichukua muda mrefu kabla ya kuamuliwa. Anataja kesi iliyomkabili aliyekuwa katibu wa lililokuwa baraza la jiji la Nairobi John Gakuo na aliyekuwa katibu wa kudumu Sammy Kirui ambayo ilichukua zaidi ya miaka tisa kuamuliwa.

Bw Gakuo na Bw Kirui walifungwa jela miaka mitatu kila mmoja na kutozwa faini ya Sh1 milioni kila mmoja kwa kutofuata sheria katika sakata ya ardhi ya makaburi ambayo jiji la Nairobi lilidaiwa kununua Athi River kwa gharama ya Sh283 milioni.

Watu wengine wawili, Mary Ng’ethe ambaye alikuwa katibu wa masuala ya sheria katika lililokuwa Baraza la Jiji la Nairobi na Alexander Musee pia walifungwa jela miaka mitatu na kutozwa faini ya Sh52 milioni na Sh32 milioni mtawalia kwa kutoa habari za uongo kuhusu suala hilo.

Wadadisi wanasema japo haki inaonekana kutendeka katika kesi za ufisadi watu walioshikilia nyadhifa za juu serikali wakikamatwa, muda wa kusikiliza kesi unafaa kupunguzwa.
Katika kesi nyingine, aliyekuwa karani wa pesa katika iliyokuwa wilaya ya Makueni Wycliff Marege Mitema alifungwa jela miaka minne na kutozwa faini ya Sh16.7 milioni kwa kujipatia mali ya umma iliyokuwa na thamani ya Sh3.8 milioni kinyume cha sheria.

Kesi hiyo ilichukua miaka tisa kuanzia 2009 hadi wiki jana uamuzi ulipotolewa akapatikana na hatia.

You can share this post!

Kampuni ya kupakia maji kiharamu yabambwa

Viongozi wagawanyika kuhusu kaunti kubadilishwa jina

adminleo