Winga chipukizi wa Kangemi alenga kufikia upeo wa Mohamed Salah
NA PATRICK KILAVUKA
Binadamu anapotia bidii katika kutumia talanta yake, huwa njia ya kupata upenyo wa maisha kwani humwezesha kuichochea kuwa kiungo muhimu cha kumsaidia hata kufikia hatima yake. Japo kila mja ana kipaji, kuwa na imani na kukitambua ni kama kujipa kifunguo cha ufanisi.
Huu ni ushauri wa mwanadimba chipukizi Benard Mutua, 17, ambaye amelivulia njuga suala la kuhakikisha amefaulu katika ndoto ya kipaji chake cha soka ndiposa awe mchezaji wa kimataifa licha ya kwamba hamna aliyekuwa mwanasoka katika jamii yao.
Winga huyo chipukizi anasukumia gurudumu la soka timu ya wasiozidi miaka kumi na saba na pia huwajibishwa jukumu kama mchezaji wa pembeni katika kikosi cha wa kubwa cha timu iyo hiyo ambayo inashiriki ligi ya Kaunti ya Shirikisho la Kandanda Nchini.
Hata hivyo, winga Mutua alianza kuondolewa ubutu wa kipawa alipojiunga na timu ya Shinning Universe chini ya kocha Derick Mudaki Muhando akiwa katika kikosi cha timu ya wasiozidi miaka kumi na moja kabla kunyakuliwa na timu ya sasa.
Chini ya kocha wake wa sasa Daniel Ywaya, anasema amenolewa na kuwa wembe wenye makali. Amempiga msasa maguu yake kwa kiwango ambacho anaweza kuhimili kucheza soka ya viwango vya juu
“Ameniongezea ncha ya ujuzi kupitia mazoezi na maelekezo ambayo anatupatia kama timu na mimi mchezaji binafsi,” anasema mchezaji huyo ambaye hucheza safu ya winga wa kushoto au kulia. Pia, usawazisha uchezaji wake katika timu pale ambapo hujukumika katika nafasi ya mashambulizi.
Kulingana na kocha wake Ywaya, anaamini kwamba mwanakabumbu huyo akiendelea hivyo, basi atakuwa na uwezo wa kusoma namba katika timu ya haiba nchini au nje ya nchi iwapo atazingatia ushauri na kuweka akili yake pamoja katika soka.
“Ni mwepesi na anajua anachopasa kufanya na wakati gani akiwa uwanja! Namtegemea katika kikosi cha kwanza katika nafasi ya winga na ameonyesha dalili za mapema kuinuka kuwa mchezaji mzuri,” anamsifa mkufunzi Ywaya huku akikariri kwamba vipaji vimo mtaani ila, ni jukumu la timu za humu nchini kuvisaka.
Wakati huu wa likizo ndefu ya ulazima kutokana na korona, mwanakandanda Mutua amekuwa akijinoa kila siku saa mbili unusu asubuhi hadi saa tatu. Hata hivyo, wikendi hujiandaa kujiweka kwenye mizani uwanjani wakati timu inapocheza michuano ya kirafiki.
Ingawa hivyo, anadokeza kwamba mlipuko wa korona ulitatanisha mazoezi hali ambayo ilipelekea viwango vya mchezo kushuka kiasi, japo sasa hali inasawazika.
Mwanasoka Mutua hufanya vimbwanga vyake vya kusakata soka akijifunza kufunga magoli, kupepeta mpira, kuudhibiti mpira, kutoa pasi za uhakika na kutoa krosi ambazo huzusha rasharasha kwenye lango la wakinzani au mazoezini wakati huu timu imeanza kujipasha misuli moto.
Anakosomea Shule ya Upili ya Edmwoka, Kangemi amekuwa kuwa moto wa pasi katika mashindano ya michezo kwa kuwa mchezaji tegemezi akimiliki nafasi iyo hiyo ya winga.
Mchezaji Mutua anasema akiwa Shule ya Msingi ya Kangemi, mwaka 2016, aliweza kusakata boli hadi kiwango cha kitaifa cha mashindano michezo ya shule za msingi ambayo yaliandaliwa Kaunti ya Nyeri akiwa katika kikosi ambacho kiwakilisha tawi la Nairobi katika mashindano hayo. Amepokea vyeti katika mashindano tokea ngazi ya mashinani hadi kitaifa jambo ambalo anajivunia.
Mutua amewahi pia kutuzwa mchezaji mahiri katika dimba la mwanakabumbu wa kimataifa, kitaifa na nahodha Victor Wanyama ambalo lilipigwa uwanja wa Shule ya St Marys, Nairobi.
Matamanio ya mchezaji huyu ni kuona kwamba anatumia maguu yake ha dhahabu hadi acheze katika ligi za hadhi nchini na ughaibuni pamoja na kuichezea timu anayoihusudu ya Liverpool kunakocheza mchezaji aliyemvutia Mohamed Salah.
Changamoto ambayo anangangana nayo kuvuka daraja ya kisoka ni vifaa vya michezo hususa buti na jezi zake.
Tamanio lake ni kwamba mchezo wa kandanda utampa fursa ya kupata udhamini wa masomo.
Angependa kuwashukuru sana wazazi na makocha ambao amepitia mikononi mwao kwa kumfungua kimawazo na kitalanta akitumainia mema kwani wamekuwa wa msaada kubwa kwake hadi umbali huu.